
DAR: Wakati Watanzania na wadau wa tasnia ya Bongo Movies wakiendelea kuomboleza kifo cha aliyekuwa mwigizaji nguli Bongo, Mohammed Fungafunga almaarufu ‘Jengua’, imebainika kuwa msongo wa mawazo kwenye maisha yake ni miongoni mwa sababu zilizohitimisha safari yake hapa duniani, IJUMAA limedokezwa.
Jengua ambaye amezikwa Desemba 16, 2020 katika Makaburi ya Mburahati jijini Dar es salaam, alifariki dunia, Disemba 15, mwaka huu nyumbani kwa mwanaye, Mkuranga mkoani Pwani.
Mkongwe huyo wa filamu nchini, inaelezwa kuwa, alipoteza maisha kutokana na maradhi ya presha na kisukari ambayo yalimsababishia kupooza (kuparalaizi).
Hata hivyo, baadhi ya madaktari waliozungumza na Gazeti la IJUMAA wameeleza kuwa, magonjwa hayo, mbali na kusababishwa na ulaji mbaya, lakini pia husababishwa na msongo wa mawazo.
Kwa mujibu wa Dk Sadick Sizya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar, miongoni mwa madhara makubwa ya msongo wa mawazo ni ugonjwa wa kisukari, shinikizo la juu au la chini la damu, kupatwa na kiharusi pamoja na magonjwa mengine ya moyo.
Dk Sizya anasema licha ya kuwa ni dhana pana, lakini magonjwa ya moyo ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo vingi duniani ambapo watu milioni 1.7 kila mwaka hufariki dunia kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2017 ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Anasema kuwa, mtu anapopatwa na msongo wa mawazo hubadilika kitabia, kuna wengine hukosa hamu ya kula wakati wengine hupenda kula kupita kiasi ambapo mwisho wa siku hupatwa na uzito kupindukia, presha na hata kisukari.
“Lakini pia msongo wa mawazo hupandisha baadhi ya homoni ambazo husababisha mapigo ya moyo kwenda kwa kasi. Sasa mapigo ya moyo yakienda kasi hayatakuwa na tija kwenye mwili wa binadamu kwa sababu badala ya kusukuma damu kwa mfumo wa kawaida, moyo hubaki kudunda tu kama ‘ku-dansi’ bila kusukuma damu kwa mtiririko sahihi.
“Damu isipofika kwa usahihi hususan kwenye ubongo ambao ndicho chakula chake, mtu hujikuta anapatwa na maumivu makali ya kichwa, kizunguzungu, kiharusi au kufariki dunia ghafla kutokana na mshtuko wa moyo,” anasema.
CHANZO HIKI HAPA
Wiki chache kabla ya kukumbwa na umauti, Jengua aliyepata umaarufu mkubwa katika mchezo wa runinga wa Kidedea kupitia Kundi la Chemchem Arts Group, alimweleza mwandishi wetu kuwa anaishi maisha magumu kutokana na soko la filamu nchini kuanguka.
“Maisha ni magumu sana, ninaumwa presha na kisukari, lakini ninajikongoja ili nipate chochote kitu, nisife njaa,” alisema Jengua.
Kutokana na hali hiyo, Dk Sizya aliongeza kuwa hali duni ya maisha huchangia watu wengi kukumbwa na magonjwa hayo yasiyoambukiza na kuondosha uhai wa watu wengi duniani.
Kwa mahojiano kamili na Gazeti la IJUMAA ambapo Jengua alifafanua namna soko la filamu lilivyomuacha hohehahe, funua makala katika ukurasa wa 6.
Stori: Mwandishi Wetu