×

Maneno ya Mwisho ya Jengua Kabla ya Kifo

KAMA ulipata bahati ya kuangalia Kipindi cha Kidedea ndani ya Kundi la ChemChem Art, kilichokuwa kinarushwa kupitia Televisheni ya ITV miaka ya 2000, kamwe huwezi kuacha kuufahamu uigizaji mahiri wa aliyekuwa mwigizaji wa Bongo Movies, marehemu Mohammed Fungafunga almaarufu ‘Jengua’.

 

Mzee Jengua amefariki dunia mwanzoni mwa wiki hii kwa maradhi ya kisukari na presha.

 

Mzee Jengua alipata umaarufu mkubwa kutokana na nafasi ya uigizaji wake kama baba mkali kama pilipili kichaa kwa watoto.

 

Aliigiza kuwa baba mkali kwa watoto kama Tabia na Sijali na kuvuta hisia kwa mashabiki huku akibeba sifa ya kupenda dogodogo kwenye mchezo huo. Nafasi hiyo ilimpa umaarufu mkubwa, lakini katika uhalisia wa mzee huyo aliyesifika pia kwa kuwa na busara na upendo wa dhati kwa jamii inayomzunguka.

 

Haya ndiyo mahojiano maalum (exclusive interview) ya mwisho ya Mzee Jengua aliyofanya na Gazeti la IJUMAA, miezi kadhaa kabla ya kifo chake;

 

IJUMAA: Mzee Jengua pole na majukumu?

JENGUA: Asante sana; tunamshukuru Mwenyezi Mungu tunaendelea na mapambano kila kukicha.

IJUMAA: Nimekukuta kazini hapa unarekodi filamu, kumbe bado zinalipa?

JENGUA: Hazilipi kiasi cha kuridhisha, lakini bado tunapambana ili tupate pesa ya kula na watoto maana maisha yameshakuwa magumu.

 

IJUMAA: Utaratibu wa malipo kwenye tasnia ya filamu sasa upoje, bado mnalipwa kwa mafungu?

JENGUA: Ndiyo, inabidi ulipwe nusu ikiuzwa ndiyo umaliziwe. Tunacheza ili tusife njaa au kugeuka kuwa ombaomba, kitu ambacho ni kibaya kabisa.

IJUMAA: Nilipata taarifa kuwa unaumwa, ndiyo maana nimekutafuta, lakini nashangaa unapiga kazi?

 

JENGUA: Ni kweli naumwa, mwili wangu hauko sawa kabisa. Kuna wakati naweza nikalala hata wiki nzima ndani, lakini mwisho wa siku ni lazima uinuke ukatafute chochote cha watoto.

IJUMAA: Nini zaidi kinakusumbua?

JENGUA: Mara nyingi, presha alafu nina sukari. Sasa natakiwa kutumia dawa mara kwa mara…ukiangalia ugumu wa maisha unazidi kutuumiza, lakini tunajitahidi.

 

IJUMAA: Mzee Jengua, upo kwenye tasnia hii kwa muda mrefu, nini ambacho unaweza kujivunia?

JENGUA: Hamna kitu zaidi ya kupita njiani na kushangiliwa na watu. Hadi sasa sina usafiri wowote, ninapanda daladala au bodaboda, sina nyumba maana nimepanga, siku nyingine mwenye nyumba anakutoa bila huruma, ila yote kheri.

 

IJUMAA: Hujawahi kufikiria kuirudisha Kidedea?

JENGUA: Natamani, lakini sasa hivi, mambo yamevurugika na wengi wameshatangulia mbele ya haki.

IJUMAA: Ulikuwa na mtoto wako mmoja wa kike alikuwa anaigiza Kipindi cha Kidedea, bado yupo?

JENGUA: Yupo, anaendelea na maisha mengine na watoto wengine wapo bado.

 

IJUMAA: Unazungumziaje tamthilia za sasa?

JENGUA: Kwa kweli tunajitahidi kidogo tunaweza kuzivunja zile za kutafsiri maana zilitupoteza kabisa.

IJUMAA: Uliwahi kutengeneza filamu yako mwenyewe?

JENGUA: Hapana, sijawahi kuwa na ya kwangu, pesa zenyewe sasa mama yangu mtihani.

IJUMAA: Naomba nikushukuru sana Mzee Jengua.

JENGUA: Asante sana na karibu tena.

 

Hayo ndiyo mahojiano ya mwisho ambayo Mzee Jengua alifanya na mwandishi wa makala haya. Baada ya mahojiano hayo, Mzee Jengua alimsindikiza mwandishi mpaka kituoni na alipopanda gari alinyoosha mkono wake wa kushoto na kutoa ishara ya kwa heri.

 

Mzee Jengua amezikwa kwenye Makaburi ya Mburahati jijini Dar, Jumatano iliynopita; sehemu aliyoishi kwa muda mrefu. Umati mkubwa ulihudhuria mazishi yake wakiwamo wadau na mashabiki wa tasnia ya filamu nchini. Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe! Amina!

IMEANDALIWA NA IMELDA MTEMA

 

Leave a Comment