
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko, leo Desemba 20, 2020, jijini Dodoma amezindua bucha ya kwanza ya nyamapori nchini kufuatia agizo la Rais John Magufuli alilolitoa mapema mwaka huu.
Uzinduzi huo umefanyika maeneo ya Chang’ombe Mtaa wa Stendi ya Zamani jijini Dodoma, ambapo Semfuko aliambatana na Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mabula Misungwi, na wajumbe wa bodi hiyo ya TAWA.

Aidha, bucha hii imekuwa ya kwanza miongoni mwa bucha 46 zilizopata usajili baada ya Kamati ya Kumshauri Kamishna kuhusu bucha za kuuza nyamapori kuridhia kufuatia kanuni ya bucha ya mwaka 2020 ambayo iliundwa baada ya tamko la Magufuli la Machi mwaka huu kuhusu kuanzishwa bucha za nyamapori Tanzania.
Wananchi wa viunga vya jiji la Dodoma leo walifurika maeneo hayo kushuhudia zoezi hilo na kufurahia fursa ya kupata kitoweo adimu cha nyamapori, ambapo wananchi walijaa katika bucha hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara aitwaye Samson Joel Kitangengi na kujinunulia kitoweo hicho.