
MKURUGENZI wa Uwekezaji wa GSM na Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Eng. Hersi Said, amesema kuwa anachoangalia zaidi ni timu yake kuendelea kupata pointi tatu kwenye kila mchezo na wala hazingatii timu zilizopo nyuma zinapata matokeo ya aina gani.
Hersi alisema wanachohitaji zaidi kwa sasa ni kuona timu haipotezi mchezo wala kufanya vibaya na ndiyo maana wakati wote yupo karibu na wachezaji pamoja na benchi la ufundi ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama kilivyopangiliwa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Hersi alisema matokeo ambayo timu yao inapata msimu huu yanamridhisha kila Mwanayanga kwa sababu timu inaongoza ligi ikiwa haijapoteza mchezo wowote, licha ya kuwa timu hiyo ina wachezaji wengi wapya na benchi la ufundi jipya, hivyo kufanya vizuri ni jambo jema kwao, huku akiongeza kuwa wao hawaangalii waliopo nyuma yao wanafanya nini, wanachozingatia ni kuona timu yao inaendelea kushinda.
“Sisi kama viongozi, tunaiandaa timu yetu kwenye mchezo unaokuja, hatuna sababu ya kuangalia aliyepo nyuma yetu anafanya kitu gani, mimi huwa sishiriki kwenye kuwaza kuhusu timu nyingine, tunaiandaa timu yetu, aliyeko nyuma atajua mwenyewe.
“Tunafurahishwa na mwenendo wa timu yetu, kwanza tunaongoza ligi tukiwa hatujafungwa, kumbuka hii Yanga ina wachezaji wengi wapya na hata benchi la ufundi lina watu wengi ambao hawakuwepo awali kwenye timu, kwa hiyo kuona watu hawa wanaungana na kupata matokeo mazuri ni jambo la kumshukuru sana Mungu,” alisema Hersi.
ISSA LIPONDA, Dar es Salaam