
KWA wakazi wengi wa mjini Moshi watakuwa ama wanamfahamu au wamewahi kumsikia Elizabeth Ng’wanza, ombaomba wa muda mrefu eneo la Posta, pembeni mwa mzunguko wa magari. Elizabeth alianza kukaa eneo hilo na kuomba kutoka kwa wasamaria tangu mwaka 1996 akitokea Urambo mkoani Tabora.
Wakati anaanza shughuli hiyo, tayari alikuwa mama wa watoto sita lakini kilichomsukuma kufanya hivyo ni ukoma alioupata. Baada ya kudumu kwa zaidi ya miongo miwili sasa, anasema muda umefika wa yeye kwenda kupumzika.
“Nimezeeka sasa, nakwenda nyumbani kwangu Urambo,” anasema bibi Elizabeth. Bibi huyo kwa sasa anaishi Njoro ambako amepanga chumba anacholipia Sh25,000 kwa mwezi, fedha anazozipata kwa kuomba.
Ili kufahamu historia na maisha yake kwa ujumla, Mwananchi limezungumza naye kuhusu shughuli zake za kuomba alizodumu nazo kwa miaka mingi. Anasema alizaliwa akiwa mzima lakini akiwa mama wa watoto sita ndipo alipata ugonjwa wa ukoma.
“Hakuna mtu mwingine mwenye tatizo hili kwetu, hata wakati nimeupata, haikujulikana niliutoa wapi kwani nyumbani walikaa upande wa baba yangu na upande wa mama yangu, kujadili kama kuna mtu katika familia hizi aliwahi kuwa na ukoma lakini hakuwepo, hivyo haikujilikana niliupata wapi,” anasema.
Bibi Elizabeth aliingia Moshi na kuanza kuomba mwaka 1996 na mwaka huu anasema utakuwa wa mwisho kwake kuendelea na shughuli hiyo.
“Nilikuja Kilimanjaro baada ya kuona naweza kupata fedha, ilikuwa mwaka 1996. Nilipanga chumba Kata ya Njoro, na kuanza kuishi huko,” anakumbuka.
Nyumba aliyokuwa akikaa awali anasema alihama baada ya mwenyewe kutaka kufanya maboresho. Alihamia nyumba nyingine anakoishi mpaka sasa akilipa Sh25,000 kwa mwezi.
“Nilipokuja na kuanza kuomba, hali ilikuwa nzuri, nilikuwa nikipata hela tofauti na miaka hii ya hivi karibuni ambapo hali imekuwa mbaya. Mwanzoni nilikuwa napata kuanzia Sh5,000 lakini sasa ni kati ya Sh1,500 hadi Sh2,000 kwa siku,” anasema Bibi Elizabeth.
Wakati mwingine, anasema anaweza kukaa siku nzima asipate chochote hivyo kutembea kwa miguu hadi Njoro anakoishi. Huanza uombaji wake kila siku saa 2:00 asubuhi na kuondoka saa 10:00 jioni.
Mafanikio
Kutokana na kufahamika kwa wengi, wapo watu wanaoamini na kusema bibi Elizabeth ni tajiri mwenye mali nyngi alizozichuma kutoka eneo analokaa akiomba msaada wa wasamaria.
Lakini mwenyewe anasema hiyo si kweli kwani alichofanikiwa maishani mwake ni kununua ng’ombe anaofuga kijijini kwao ambako wanasimamiwa na watoto wake, wanaofanya shughuli za kilimo pia.
Anasema hutumia sehemu ya fedha anazopata kuwalipia wajukuu wake ada ya shule na kuwanunulia mahitaji mbalimbali kama vile sare na vifaa vya shule, vitabu, madaftari na kalamu kuhakikisha wanapata elimu. Pamoja na ukweli huo, anasema kuomba ndiyo kazi anayoitegemea kumwingizia kipato cha uhakika.
Kurudi Urambo
Bibi Elizabeth anasema anatarajia kuondoka Moshi kurudi nyumbani kwake Urambo Januari 5 mwakani na amefanya uamuzi huo kwa kuwa amezeeka sasa.
“Natarajia kuchukuliwa na mwanangu kwenda Urambo, sitegemei kurudi tena. Nakwenda nyumbani kupumzika, vitu nilivyo navyo vile vidogo vidogo vinavyofaa kubeba nitabeba lakini vingine ambavyo havifai kama kitanda, nitavipiga bei,” anasema.