
DAKTARI wa Yanga, Shecky Mngazija, amejibu tuhuma za baadhi ya mashabiki na wadau wa timu hiyo za kumchezesha beki wa timu hiyo, Lamine Moro akiwa majeruhi kufuatia kutokimbia vizuri uwanjani.
Lamine ni miongoni mwa wachezaji bora ndani ya kikosi cha Yanga lakini amekuwa akisumbuliwa na goti. Katika mechi mbili zilizopita, Lamine alionekana akicheza akiwa anachechemea, licha ya kufunga na kuisaidia Yanga kupata ushindi wa mabao 5-0 na 3-1, dhidi ya Mwadui na Dodoma Jiji, mtawalia.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mngazija amesema kuwa, mara nyingi Lamine amekuwa akipatwa na maumivu anapokuwa uwanjani baada ya kutoneshwa na si kwamba amekuwa akichezeshwa akiwa majeruhi.
“Lamine sio mchezaji majeruhi hata kidogo, si kwamba tunamchezesha akiwa majeruhi, yupo fiti ila kinachotokea uwanjani ni kwamba amekuwa akitoneshwa, ndio amekuwa akipatwa na maumivu, sio kwamba amekuwa akichezeshwa akiwa na maumivu.
“Lamine ni mchezaji profesheno, hawezi kukubali kucheza akiwa na majeraha mwilini, anacheza akiona yupo fiti, hivyo tuhuma hizo si za kweli,” alisema Mngazija.
KHADIJA MNGWAI, Dar es Salaam