×

Dkt. Gwajima Aanza na Wakurugenzi Afya

WAKURUGENZI wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wametakiwa kuainisha changamoto na mahitaji yote yanayohitajika ili kuakisi na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwezesha kuleta maendeleo katika sekta ya afya nchini.

 

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Wizara hiyo,  Dkt. Dorothy Gwajima. wakati wa majumuisho ya kikao-kazi cha wakurugenzi wa wizara hiyo na taasisi zake waliokutana jijini Dodoma na kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini.

 

Amesema kuwa licha ya maelekezo mengi ambayo yamekwishatolewa kazi kubwa ambayo wanatakiwa kufanya ni kuandaa vibango kitita vya changamoto zote walizonazo katika taasisi zao na namna gani wanaweza kuzitatua katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

 

“Mnapoondoka hapa mnajua tunazo kazi za kufanya, mkaweke changamoto zenu katika madaraja na kuainisha ni changamoto zipi sisi tunatakiwa kuhusika na zipi nyinyi na taasisi zenu mnatakiwa kuhusika na nini kifanyike na kwa njia zipi kwa kujumuisha ilani kwa mwaka wa kwanza hadi wa tano,” alisisitiza Gwajima.

 

Aidha,  aliwataka wakurugenzi hao kutokaa na changamoto bali wanapaswa kufanya vitu kuendana na mwelekeo wa sasa ili kuleta faida na tija kwa taifa hususani kwenye sekta ya afya.

 

“Ni lazima tuakisi hayo ambayo kielimu na kiuwezo tumeyafikia kwa kuzingatia dhana nzima ya mikakati ya utekelezaji wa sera ya afya, mkakati wa tano wa sekta ya afya, mkakati wa kufikisha afya kwa wote pamoja na maeneo ya kipaumbele ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika sekta ya afya,” aliongeza.

 

Pia alisema kuwa ili kuweza kutekeleza hayo kwa ufanisi mkubwa wizara yake inataka kuwa na uratibu anuwai kwa kila mkurugenzi wa taasisi kuwasilisha uelekeo wake na kufunga nao mkataba ili kuweka mazingira rafiki kwa kufikia na kutekeleza ilani.

 

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kikao hicho kimelenga kufahamiana na kuwa timu moja katika uwajibikaji na namna gani wanakwenda kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta ya afya nchini.

 

Amesema kukaa kwa pamoja kunasaidia kupanga na kufanya maamuzi yaliyo sahihi ili kuweza kuwatumikia wananchi kwa pamoja na ndiyo maana wananchi wameiamini serikali hii, hivyo timu waliyonayo ni nzuri na wataweza kufanya kazi kubwa zaidi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Leave a Comment