
RAIS John Magufuli amemwapisha Jaji wa Mahakama ya Rufani, Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi, kuwa Kamishna wa Maadili, leo Desemba 24, 2020, Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya uapisho huo, Magufuli amewataka watumishi wa umma kutowasilisha fomu zao za maadili (fomu za mali na madeni kila mwaka) kwa Tume ya Maadili kupitia njia ya mtandao kwani itaondoa usiri na utakatifu wa chombo hicho.
“Najua leo ni Desemba 25 na Desemba 30 ndiyo mwisho wa sisi watumishi wote kurudisha fomu, ndiyo maana nilitaka kabla ya Desemba 30 niwe nimeshateua Kamishna wa Maadili ili kusiwepo na kisingizio, nina uhakika sote tunaowajibika kuzijaza hizo fomu tutawasilisha kwa wakati. Wewe utakuwa refarii wa maadili kwa sisi sote watumishi, na wewe ndiyo bosi wetu, kwa hiyo nikutakie utendaji mwema.
“Unaweza ukafanya mambo mengine yote kwa njia ya mitandao lakini ujaze fomu… kwa mfano Katibu Mkuu Kiongozi aeleze mali zote alizo nazo, ajaze, mfano ana nyumba ndogo ambayo mke wake haijui, ule usiri na utakatifu wa idara hiyo mnaupoteza.
“Ukishajaza usi-scan na kuzirudisha tena mtandaoni, spika huwa analeta kwangu, wewe (Kamishna wa Maadili) unaleta kwangu na mimi naleta kwako, wanaojaza wengi, Ma-DC, Ma-RC, Ma-RAS, ni vyema wa-download, wajaze na kuzirudisha mahali inapotakiwa.
“Lazima pawe na usiri wa fomu hizi hackers (wadukuzi mtandaoni) wapo wengi akishajua programu hizi ana-edit wewe umejaza milioni 10 anakujazia una milioni 100, baadaye unaulizwa ulizaja milioni 100 na umesaini, hivyo usikubali kurudisha fomu hizi kwa njia ya mtandao.
“Watumishi wenzangu tujitahidi kuwasilisha fomu za maadili, nafahamu wengi wenu hapa hamjajaza fomu hizo, hata mimi ya kwangu nilikuwa sijajaza, lakini nitafanya hivyo mapema iwezekanavyo ili nikufikishie (Kamishna wa Maadili) kwa mujibu wa sheria zilizowekwa…
“Nawatakia Krismasi na Mwaka Mpya mwema, siku mbili au tatu ukikimbia kwenda kusherehekea Xmas na mama yako siyo mbaya, au kula mwaka mpya na babu yako si vibaya, wengine mtaenda kutambika kama Wahehe…. isipokuwa waliozuiwa na Waziri Mkuu wanaotakiwa kuwajibika wabaki,” amesema Magufuli.