×

Funga Mwaka 2020… Mondi Kicheko, Kiba Maumivu

AMA kweli mwaka huu ulikuwa kicheko kwa msanii wa Bongo fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ au Mondi huku wasanii wenzie akiwamo mshindani wake mkubwa katika anga ya muziki huo, Ali Kiba wakiugulia maumivu.

Licha ya kuwepo kwa changamoto za ugonjwa wa Corona ambao umeathiri pakubwa sanaa na harakati nyingi za kimaisha duniani mwaka 2020, Mondi amekuwa kwenye mafanikio makubwa yaliyowaacha mbali washindani wake.

 

Mbali na Mondi kama bosi wa Lebo ya Wasafi Classic Baby ‘WCB’ wasanii waliopo chini yake kama Zuhura Othman ‘Zuchu’, Mbwana Kilungi ‘Mbosso’ na Raymond Shaban ‘Rayvanny’ nao wamefanya vizuri kimuziki kwenye mwaka huu ambao umefikia ukingoni.

 

NGOMA YA KUFUNGIA MWAKA

Wakati Mondi akifungia mwaka na wimbo wa Waah aliomshirikisha mwanamuziki nguli kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomide kwa kuweka rekodi ya ajabu kwa kutazamwa na watu zaidi ya milioni 24 kwa muda mfupi wa wiki nne, Kiba ameachia ngoma yake mapema wiki hii ambayo hata hivyo bado haijakimbiza na kuweka rekodi.

Kiba aliachia ngoma iliyokwenda kwa jina la ‘Nakupenda’ akiwa amemshirikisha Disc jockey ‘Dj Sbu’ kutoka Afrika kusini.

 

TUZO

Mapema mwezi huu Mondi alitunukiwa tuzo ya Msanii Bora wa Kiume wa Mwaka kwenye tuzo zinazotolewa na waandaji AEAUSA wa nchini Marekani.

Msanii mwingine kutoka Lebo ya WCB aliyechukua tuzo hizo ni ‘Rayvanny’ ambaye amechukua tuzo ya Msanii Bora wa Kiume ukanda wa Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika.

 

Msanii mwingine wa Bongo aliyetwaa tuzo hizo za AEAUSA ni Faustina Mfinanga ‘Nandy’ ambaye alitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Mwaka.

Hata hivyo, Kiba ambaye ni mkongwe katika muziki wa Bongofleva, licha ya kuchuana vilivyo na Mondi, hakuambulia tuzo yoyote mwaka huu.

 

Badala yake akipiga stori na gazeti dada na IJUMAA, alisema suala la tuzo kwake sio kipaumbele.

Kiba alienda mbali zaidi na kusema kuwa waandaaji wa tuzo mbalimbali hucheza michezo michafu na kuwashindisha wasanii ambao hawastahili.

 

KUWABEBA WASANII

Katika mojawapo wasanii ambao Mondi anajivunia kuwaibua mwaka huu na kudhihirisha umahiri wao, ni Zuchu.

Zuchu aliibuka Aprili mwaka huu kipindi ambacho Corona imepamba moto lakini cha ajabu alitoboa na kupata mafanikio makubwa ya kisanaa.

Zuchu alimshirikisha Mondi katika ngoma za Cheche na Litawachoma ambazo kwa pamoja zilifanya vizuri mwaka huu.

 

Wakati Mondi akitamba kumuibua Zuchu, upande wa pili Kiba ambaye ni mmoja wa wasanii wenye hadhi ya kupambanishwa na Mondi, alikimbiwa na msanii mkali aliyekuwa kwenye himaya yake.

Ibrah alimkacha Kiba na kuelekea Konde Gang ambayo inamilikiwa na Rajabu Abdul ‘Harmonize’.

 

UWEKEZAJI

Katika kipindi cha mwaka huu pekee, Mondi ameendelea kuweka alama baada ya kutambulisha vitega uchumi mbalimbali alivyomudu kuviweka kwenye himaya yake.

Aprili mwaka huu Mondi alionesha mjengo wa hoteli alioinunua huko maeneo ya Mikocheni Dar es Salaam. Pia Novemba mwaka huu aliweka wazi kumnunulia mama yake mjengo mwingine huko Masaki.

 

Mbali na hayo, mwaka huu Mondi alitimiza haja ya ndoto ya maisha yake baada ya kununua gari kali analolipenda.

Mondi alinunua gari aina ya Rolls Royce iliyodaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 800.

Aidha, kwa upande wa Alikiba kubwa lililovuja mwaka huu ni ghorofa la msanii huyo lililopo huko Tabata, Dar es Salaam.

 

Licha ya kuwa Disemba mwaka jana Kiba aliweka wazi mipango ya kufungua studio kali, hadi sasa hakuna mwendelezo wowote hali inayothibitisha kuwa mwaka huu ulikuwa wa maumivu kwake na wasanii wengine walioshindwa kutimiza baadhi ya mahitaji yao.

 

SHOO ZA KUFUNGA MWAKA

Wakati Diamond akipiga shoo ya kufunga mwaka huko Sudani kusini, Alikiba alitarajiwa kupiga shoo nchini Burundi lakini kwa bahati mbaya ikabuma.

 

Inaelezwa kuwa shoo ya Mondi huko Sudani ilijaza watu wengi na kuacha historia ya kipekee, lakini kwa upande wa Alikiba inaelezwa kuwa wananchi wa Burundi waliokuwa wamekata tiketi za viingilio katika shoo yake hiyo waliondoka uwanjani kwa hasira baada ya msanii huyo kushindwa kuperfom.

Stori: Mwandishi Wetu, Dar

Leave a Comment