
KAJALA Masanja wengi wao wanapenda kumuita ‘ ‘Kay’ wengine wanamuita boss lady, amewakata kilimilimi baadhi ya watu wanaosema kuwa mtoto wake Paula ambaye amezaa na prodyuza maarufu Bongo, Paul Matthysse ‘P Funk’ kuwa ataolewa mapema lakini yeye amesema kuwa mtoto wake huyo hawezi kuolewa mapema.
Kajala amesema anataka asome mpaka mwisho.
Akipiga stori na gazeti la Risasi Jumamosi, Kajala anasema anaona wazi maisha aliyopitia baada ya kuolewa mapema hivyo anatamani kabisa kuona mtoto wake huyo anapata mafanikio kwenye kusoma.
Pamoja na jambo hilo, Kajala amefunguka mambo mengine mengi.
Zaidi, ungana nami kwenye mahojiano yafuatayo hapa chini:
ANAISHIJE NA MTOTO WAKE HUYO?
“Wengine hawawezi kujua ni jinsi gani ninaishi na Paula. Unajua mimi ni mama kijana lakini lazima mtoto wangu anitii na aishi vile ninavyotaka au ninavyomuelekeza na akinizingua ninamfundisha adabu.
“Lakini pia kuna wakati tunaweza kuzungumza tukacheka na kutaniana.”
ANAMPIGA AKIMKOSEA?
“Tena siyo kitoto, anaponikosea mimi ni mkali sana. Siku zote nilifundishwa na mama yangu ‘akupigaye ndiye anayekufunza’.
Paula anapokosea ninamfundisha na panapostahili kumchapa nafanya hivyo japokuwa siyo mara nyingi maana Paula ni mkubwa sasa, tunakaa tunazungumza na ananielewa vizuri na kuna kipindi tunakuwa marafiki sana.”
VIPI KUHUSU MALEZI YA KWAKE MWENYEWE BILA BABA?
“Ni magumu kwa sababu sidhani kama kuna mama anapenda kulea mtoto bila baba ila kwa sababu imenilazimu kuwa hivyo, sina jinsi na uzuri Mungu kanipa nguvu ya kusimama kama mama ingawa huwa anakwenda kwa baba yake anapopata nafasi.”
ANAZUNGUMZIAJE MWANAYE KUOLEWA MAPEMA?
“Hapana sipendi kabisa aolewe mapema ingawa ni mtoto wa kike, nataka asome mpaka aseme mwenyewe basi kwa sababu mimi nilipita huko hivyo nataka tu elimu iwe mkombozi wake na si kitu kingine.”
VIPI KUMVALISHA MAVAZI YA KIMJINI?
“Sidhani kama kuna nguo ya ajabu ambayo ninamvalisha Paula, lakini najaribu kumuweka mtoto wangu kisasa zaidi na sidhani kama mavazi yanaweza kufanya tofauti au kumbadilisha tabia maana ninamkuza ili vitu vingine aone vya kawaida tu.”
KWA NINI HAPENDI KUONGOZANA NAYE?
“Nafikiri siyo sahihi sana kila sehemu niende na mtoto wangu, si vizuri ajue kila kitu ninachofanya mama yake, kuna mipaka yake, kuna sehemu ninapaswa kuwa naye, tukae tule, aogelee na mambo mengine…”
ANAMCHUKULIAJE PAULA?
“Paula ni roho yangu kabisa, ninampenda mno na ni mtoto ambaye amenifundisha maisha vilivyo na pia ni mtoto wa historia ya maisha yangu.”
ANAMZUNGUMZIAJE BABA WATOTO WAKE?
“P Funk namheshimu kama mzazi mwenzangu, kwa sasa yeye ana mke wake na maisha yake na mimi nina maisha yangu. Muhimu tunamlea mtoto wetu vizuri basi tunamshukuru Mungu.”
ANAZUNGUMZIAJE KUOLEWA TENA?
“Mh! Kwa sasa napambana na maisha yangu ili mwanangu pia asome na pia aishi vizuri. Kama unavyojua mimi nilishaolewa na tuliachana hivyo kwa sasa sifikirii sana kuhusu kuolewa.”
MAKALA: IMELDA MTEMA