
UONGOZI wa Yanga umesitisha mipango ya kumsajili beki na nahodha wa Biashara United, Abdulmajid Mangaro aliyekuwemo kwenye mipango ya kusajiliwa na timu hiyo.
Yanga imepanga kuongeza beki mmoja wa kati mzawa katika usajili huu wa dirisha dogo na Mangaro alikuwemo kati ya wanaowaniwa.
Hiyo ni katika kuiongezea nguvu safu ya ulinzi ya Yanga ambayo inaongozwa na manahodha Lamine Moro na Bakari Mwamnyeto ambayo hadi hivi sasa imeruhusu mabao matano pekee katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara, wakicheza michezo 18.
Taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mrundi Cedric Kaze ndiye aliyekataa kusajiliwa kwa beki huyo katika usajili huu wa dirisha dogo ambalo litafungwa Januari 16, mwaka huu.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa sababu kubwa iliyomfanya Kaze asitishe mipango hiyo ya usajili ni kutokana na kukosa kasi. Pia hana maamuzi ya haraka wakati akiwa na mpira.
Aliongeza kuwa kocha na uongozi wa timu hivi sasa upo katika mipango hiyo ya kumpata beki mwingine mzawa mwenye uwezo na uzoefu wa ligi kwa lengo la kuwapa ushindani mabeki Lamine na Mwamnyeto, licha ya kuwepo akina Said Makapu na Abdallah Shaibu ‘Ninja’. “Kikubwa kinachomfanya Kaze amkatae Mangaro ni kutokana na kukosa kasi, pia hana maamuzi sahihi wakati akiwa ana mpira katika kuokoa mpira golini kwake.
“Kabla ya kumsajili kocha Kaze alitafuta video za mechi ambazo amezicheza beki huyo na kuona upungufu wake huo ambao kwake ameona hatakuwa na msaada.
“Viongozi kwa kushirikiana na kocha hivi sasa wanafanya jitihada za kumpata beki mwingine mwenye uwezo zaidi ya akina Lamine na Mwamnyeto kwa ajili ya kuwapa ushindani,” alisema mtoa taarifa huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alizungumzia hilo kwa kusema: “Suala la usajili tumemuachia kocha ambaye yeye ndiye anapendekeza mchezaji na kutuletea jina lake na sisi kama uongozi tunawezesha katika kutoa fedha pekee, hivyo hilo suala lipo kwa kocha.”
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam