
MBUNGE wa jimbo la Chalinze mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete, amefika nyumbani kwa familia ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Msasani jijini Dar es Salaam kuhani msiba, kufuatia kifo cha Rosemary Nyerere aliyefariki dunia Januari 1, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kikwete pia amesaini kitabu cha maombolezo na kutoa pole kwa familia ya Nyerere wakiwemo watoto na wajukuu wa Nyerere.
Awali akitoa pole kwa mtoto wa Nyerere – Makongoro Nyerere – Kikwete ameeleza kuwa familia ya Nyerere imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha Rosemary, hivyo anaungana na familia hiyo katika kipindi hicho cha majonzi.
“Tunaungana kwa pamoja katika msiba huu mzito, hakika umetugusa sote, kwa niaba ya familia yangu pamoja na Wanachalinze tunatoa salamu za pole kwa wanafamilia ya Nyerere,” amesema Kikwete.
Rosemary alikuwa miongoni mwa watoto saba wa Nyerere na anatarajiwa kuzikwa kesho Jumatano, Januari 6, 2021 katika Kituo cha Hija, makaburi ya Pugu Misheni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.