
HATIMAYE Simba wameingilia kati usajili wa beki wa kushoto wa Namungo, Edward Charles Manyama ambaye yupo katika mazungumzo na viongozi wa Yanga ambao wanataka kumsajili beki huyo katika dirisha hili dogo.
Manyama amekuwa katika kiwango kizuri ndani ya Namungo ambalo limemfanya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachojiandaa na michuano ya CHAN kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya Afrika.
Chanzo chetu cha uhakika kutoka Simba kililiambia Championi Jumatatu kuwa kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameuomba uongozi kupitia dirisha dogo la usajili uweze kusajili beki mwingine wa kushoto ili aweze kusaidiana na Mohammed Hussein na Gadiel Michael ambapo viongozi wa timu hiyo wamelipendekeza jina la Manyama.
“Uongozi umepokea ripoti ya mwalimu ambayo inahitaji ongezeko la beki mwingine wa kushoto ili aweze kusaidiana na Mohammed Hussein pamoja na Gadiel Michael ambapo uongozi umeona kuwa Edward Manyama ni mtu sahihi wa kuongezeka katika kikosi.
“Tayari mazungumzo yamekwishaanza na meneja wa mchezaji huyo ili kuona tutampataje mchezaji huyo ambaye kama atapatikana basi tutakuwa tumenufaika sana kwa kuwa anaweza kucheza katika nafasi ya kiungo wa chini,” kilisema chanzo hiko.
Naye Edward Manyama aliliambia Championi Jumatatu: “Kwa sasa siwezi kuzungumza kitu chochote juu ya usajili wangu kwani maneno yameshakuwa mengi kuhusu kuhitajika na baadhi ya timu na ukiangalia kwa sasa mimi ni mchezaji halali wa Namungo, hivyo siwezi kuzungumzia kuhusu mambo ya usajili.”
Manyama kwenye ligi kuu msimu huu akiwa na Namungo, amefanikiwa kufunga bao moja na kutengeneza mabao mengine matatu kwa washambuliaji wa Namungo.
MARCO MZUMBE,
Dar es Salaam