×

DStv Yaikabidhi Jezi Global FC, Kucheza Januari 31

Meneja wa Masoko wa DStv Tanzania, Shelukindo (kulia) akimkabidhi jezi Mhariri Mtendaji wa Global Group, Saleh Ally.

UONGOZI wa DStv Tanzania leo Januari 8, 2021,   umeikabidhi timu ya Global FC jezi za nyumbani na ugenini kwa ajili ya michezo ya kirafiki  na mashindano mengine ambayo itashiriki  kwa msimu wa 2021.

 

Makabidhiano hayo yamefanyikafika katika ofisi za Global Group zilizopo Sinza-Mori jijini Dar es Salaam ambapo zitatumika rasmi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya DStv Tanzania unaotarajiwa kuchezwa Januari 31,2021.

Mkuu wa Masoko wa DStv Tanzania, Ronald Baraka Shelukindo, amesema kuwa lengo kubwa la mchezo huo ni kuongeza ushirikiano zaidi kwa mwaka 2021.

…Wakionyesha jezi hizo.

Akizungumza na wafanyakazi wa Global Group wakati wa makabidhiano, Shelukindo alisema kazi kubwa ya DStv ni kuendelea kuwa karibu na wale ambao wanafanya nao kazi kila siku.

…Saleh Ally  akielezea jambo.

“Tumekuwa tukifanya kazi na Global Publisher kwa muda mrefu, siyo kwa kuwa tuna mchezo nao wa kirafiki tu mwishoni mwa mwezi huu, Januari, hapana ni muda mrefu kwa kuwa kazi zetu na kile ambacho wanakifanya wao vinategemeana.

“Huwezi kuzungumzia masuala ya michezo kwa sasa bila kuitaja DStv kwa kuwa inabeba kila kitu mpaka masuala ya movie na kila mtu anafurahia huduma zetu, hivyo mchezo tutacheza nao na tukiwafunga wataendelea kufurahia huduma zetu. Wateja wetu wazidi kutupa sapoti mwaka huu mpya wa 2021 tunakuja kivingine,” alisema.

Timu ya DStv wakitambulishwa kwa Meneja wa Global Radio, Bori Mbaraka (kulia),

Naye Mhariri Mtendaji wa Global Publisher, Saleh Ally alisema kuwa watazidi kuongeza ushirikiano na DStv kwa kuwa wamekuwa nao kwa muda mrefu, jambo ambalo limewafanya wamekuwa ni familia.

 Shelukindo akichangia moja ya mada katika kipindi cha Kata Mbuga kinachorushwa na Global Radio.

“Kwa sapoti ambayo tunapeana na DStv ni kubwa na inatufanya nasi tunazidi kuongeza nguvu katika kuboresha familia hii ambayo ni bora na yenye furaha, ninaona wametuletea jezi ilhali wanajua kwamba timu yetu inakwenda kuwafunga, ila yote kwa yote huu ni mwanzo ndani ya 2021,” alisema Ally.

Saleh Ally akitoa pongezi kwa Dstv katika kipindi cha Kata Mbuga.

Wakati huohuo, nahodha wa Global FC, Wilbert Molandi,  amesema sapoti waliyoipata kutoka DStv ni kubwa na wanaamini kwamba wataendelea kushirikiana.

“Tutazidi kushirikiana na DStv kwa kuwa wamekuwa bega kwa bega katika kazi ambazo tunazifanya, ni familia moja,  hivyo lazima tuzidi kuongeza nguvu ukizingatia kwamba mwaka 2021 unaanza. Kwenye mchezo wetu wachezaji wetu wapo vizuri kutakuwa na burudani,” alisema.

STORI NA LUNYAMADZO  MLYUKA | PICHA NA IBRAHIM MUSSA -GPL

Leave a Comment