
MBUNGE wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo amekutana na Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Get Mweli pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda kujadili maendeleo ya elimu katika halmashauri hiyo.

Katika kikao hicho Shigongo amemuomba Naibu Katibu Mkuu huyo kuongeza walimu katika shule za sekondari pamoja na za msingi kwani idadi ya wanafunzi katika shule za halmashauri hiyo ni kubwa ikilinganishwa na uwiano wa walimu jambo linawafanya wanafunzi kushindwa kupata elimu stahiki.

“Wanafunzi wamekuwa wakifanya vibaya katika mitihani yao ya kitaifa na kuonekana hawana akili, lakini ukweli ni kwamba kuna wanafunzi wengi tu wenye akili tena nyingi sana wanaosoma shule za vijijini, lakini shida kubwa imekuwa ni mazingira duni ya kujifunzia na kufundishia pamoja na upungufu wa walimu kwenye shule zetu,” amesema Shigongo.

Katika suala la ujenzi wa madarasa Shigongo amesema, wananchi wanajitolea sana juu ya maendeleo hivyo serikali ikiongeza nguvu, sekta ya elimu ya Buchosa itapanda na wanafunzi watafaulu kwa kiwango kikubwa.

Kwa Upande wake, Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Gerald Mweli amesema lengo la ziara yake ni kuja kuona hali na mazingira ya elimu ilivyo Buchosa ili serikali iweze kupanga mipango mikakati ya kuboresha elimu katika halmashauri hiyo.
NA IDD MUMBA | GLOBAL PUBLISHERS, BUCHOSA