
WAKATI Rais Mteule wa Marekani Joe Biden akitarajiwa kuapishwa Jumatano Januari 20, Majimbo yote 50 ya Marekani yamewekwa katika hali ya tahadhari kutokana na uwezekano wa maandamno ya ghasia wikendi hii, kabla ya uapisho huo.
Vikosi vya ulinzi wa kitaifa vimetumwa kwa wingi katika mji wa Wshington DC ili kuzuia kuzuka kwa ghasia mbaya za wiki iliopita.
Shirika la FBI limeonya kwamba huenda kukatokea maandamano ya ghasia yatakayotekelezwa na wafuasi wa rais Trump katika majimbo yote 50.
Wakati huohuo, kundi la Biden limeweka mipango kufutilia mbali baadhi ya sera zilizoweka na rais Trump.
Muda mfupi baada ya Joe Biden kuingia katika Ikulu ya Whitehouse , ataanza kubadili baadhi ya maagizo yaliowekwa kando na Trump kama njia ya kuonesha tofauti kati ya utawala unaoondoka na unaoingia , kulingana na barua ilioonekana na vyombo vya habari vya Marekani.
Eneo kubwa la Washington DC litafungwa kabla ya sherehe ya kuapishwa kwa Joe Biden huku maelfu ya maafisa wa kikosi cha ulinzi wa kitaifa wakisambazwa kila mahali.
Barabara ambazo zipo karibu na majengo ya Bunge , eneo ambalo ambalo zilitokea ghasia mbaya za tarehe Januari 6 yamezuiwa na vizuizi na ua wa chuma.
Eneo la National Mall ambalo hushuhudia maelfu ya watu kwa sherehe hiyo ya kuapishwa kwa marais limefungwa kutokana na ombi la kikosi cha upepelezi kitengo kinachomlinda rais.
Kundi la Biden tayari limewataka Wamarekani kutosafiri hadi mji mkuu wa taifa hilo kwa sherehe hiyo kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Maafisa wamesema kwamba raia wanapaswa kutazama sherehe hiyo kutoka majumbani.