
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema askari watakaoshindwa kuwabaini wahamiaji haramu hususani maeneo ya mipakani wanapoingilia watawajibishwa.
Amesema kitendo cha wahamiaji haramu kukamatwa maeneo mbalimbali ndani ya nchi, ambayo siyo mipakani ni kutokana na kuwepo na mawakala wanaofanikisha wahamiaji hao kuingia nchini.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wa uhamiaji katika kambi mpya ya mafunzo ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, Simbachawene amesema watawashughulikia askari wote wanaoingia katika mikoa ya mipakani ambapo wanaingia kwa mara ya kwanza wahamiaji hao.
“Wahamiaji haramu kama tukiwakata Morogoro na wakasema wameingia hapa Mkinga, sisi hatushughuliki na wale wa Morogoro, tutashughulika na waliopo Mkinga na Tanga, tuwahoji wamepitajepitaje wahamiaji hawa haramu?” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “Pia tutawauliza polisi, ilikuwaje msiwaone wahamiaji hawa haramu maana ‘barrier’ zote zenu, hawa hawatembei kwa miguu, walipanda gari, walipandia wapi gari, na kama wakituambia walipanda gari, hawa watu wote (polisi na uhamiaji) wapo kwenye wizara yangu, wote nitafagia.”
Pia amesema mipaka ya nchi lazima ilindwe kwa sababu askari wana taaluma zote za kijeshi za kupambana na wahamiaji haramu, hivyo kitendo cha kupita mipakani na kukamatwa maeneo ya ndani ya nchi ni hatari na kama adui basi atakuwa ameishambulia nchi.
“Ukiona msafara wa wahamiaji haramu umefanikiwa kutoka point A mpaka B ujue kuna mawakala, kutoka point B mpaka C ujue kuna mawakala, wale watu wanaokuja ni wageni, wanawezaje kupita point A mpaka Point B, kama wamefanikiwa kufika mpaka Dar es Salaam wakakamatwa Tegeta au Mbezi, maana yake tumeshapigwa kama ni adui, lazima tuwe makini kila mtu katika eneo lake,” alisema Simbachawene.
Aidha, aliwataka wanafunzi wa kambi hiyo kuzingatia masomo ya uhamiaji wanayopewa yakiwemo ya uongozi na utawala, masuala ya kikonsula, mawasiliano, ulinzi wa kujihami na gwaride.
“Mafunzo mtakayoyapata kutoka kwa wakufunzi wenu yanalenga kudumisha nidhamu ya kijeshi, uzalendo, utii, uwajibikaji na maadili bora, ninawaomba zingatieni tunu hizo katika kipindi hiki chote cha mafunzo, kwani ndiyo silaha kubwa kwa askari na katika uongozi bora,” alisema.
Naye Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI), Dkt. Anna Makakala, alisema mafunzo katika kambi hiyo mpya, yanajumuisha askari na maafisa wa uhamiaji 287, wanawake 81 na wanaume 206, ambapo mchanganuo wa kozi ya Mrakibu Msaidizi wapo 32, Mkaguzi Msaidizi wapo 112, kozi ya Sajini 42 na kozi ya Koplo wapo 101.
“Mheshimiwa mgeni rasmi napenda kukujulisha kuwa Kambi ya Mafunzo ya Boma Kichaka Miba inamilikiwa na Idara ya Uhamiaji na Chuo cha Kikanda (TRITA) kilichopo Mjini Moshi, kambi hii ina ukubwa wa ekari 395 na tayari tumekabidhiwa hatimiliki, ambapo ujenzi wa kambi hii ulianza rasmi mwezi Julai, 2020 na kiasi kilichotumika ni shilingi milioni 140. Fedha hizi zimetokana na michango ya hiari ya askari na maafisa wa uhamiaji ambao walichangia Shilingi milioni 81 na wadau rafiki wa uhamiaji walichangia milioni 59 vikiwemo vifaa vya ujenzi” alisema Makakala.
Aidha, Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela, aliwataka waatu waishio jirani na kambi hiyo kutoa ushirikiano kwa kambi hiyo, na pia wasivamie maeneo ya kambi hiyo wakiona ni vichaka wakafikiri ni eneo ambalo halina mwenyewe.
Na Mwandishi Wetu, MOHA.