
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo Jumanne 19, 2021 itaikabili Zambia katika mchezo wa kwanza wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), huku ikiwa na matumaini kibao ya kuibuka na ushindi.
Licha ya kuwa na matumaini hayo, lakini Taifa Stars imepanga kuingia kwa tahadhari kubwa kutokana na wapinzani wao kuonekana si wa kuwabeza.

Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Seleman Matola, amesema kuwa, wana matumaini ya kufanya vizuri katika michuano hiyo, huku wakiwa na tahadhari kubwa kutokana na ushindani uliopo.
“Hii ni michuano mikubwa, kila timu inahitaji kufanya vizuri na imekwenda kwa ajili ya lengo moja tu la kushinda, hivyo tunajipanga kwa upande wetu kuona tunafanikiwa kufanya vizuri na kushinda mchezo wetu wa kwanza.
“Tunajua wapinzani wetu wapo vizuri lakini pia kwa upande wetu tunahitaji kujituma na kuonesha kiwango ili tushinde na kufanya vizuri katika mashindano hayo,” alisema Matola.Katika michuano hiyo iliyoanza Jumamosi iliyopita na kushirikisha timu 16, Taifa Stars imepangwa Kundi D na timu za Zambia, Guinea na Namibia.