
UPANDE wa Mashtaka katika kesi inayowakabili wabunge wa viti maalum akiwemo, Halima Mdee na Ester Bulaya na wafuasi 27 wa Chadema wanaokabiliwa na kesi ya jinai yenye mashtaka saba likiwemo la kukaidi amri halali na kuharibu geti la gereza la Segerea kutoa samasi kwa washtakiwa watatu ambao hawakuwepo kwa ajili ya kutoa maelezo ya kwanini wasifutiwe dhamana.
Hayo yamejiri mapema leo wakati kesi hiyo ilipotajwa ambapo wakili wa serikali, Ester Martin, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ameomba mahakama kutoa samasi hiyo ili washtakiwa waweze kufika mahakamani na kutoa maelezo.
Washitakiwa hao ambao upande wa mashtaka umeomba kutolewa samasi ni mshtakiwa wa 8,15 na 16 ambao hawakufika mahakamani. Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 15, mwaka huu kwa ajli ya kuendelea na usikilizwaji.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Jesca Kishoa, aliyekuwa Meya wa Ubungo Boniface Jacob, aliyekuwa Diwani wa Tabata Patrick Assenga na Mshewa Karua.
Wengine ni Khadija Mwago, Pendo Mwasomola, Happy Abdallah, Stephen Kitomali,Athumani Hassan, Omary Milodo, Emmanuel Ignastemu, Stephen Kitomali, Hamis Yusuph, Juma Juma, Mustafa Lada, Emmanuel Zakaria na Steven Ezekiel.
Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Machi 13, 2020 washitakiwa hao wakiwa katika gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, isivyo halali na kwa makusudi walikaidi amri iliyotolewa na askari B 3648 SGT John ambaye aliwataka wahusika hao kuondoka eneo hilo la magereza na alikuwa akitimiza wajibu wake aliyopewa.