
WATAALAMU kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) wameanza kuchunguza chimbuko la virusi vya corona kwa kutembelea hospitali moja mjini Wuhan nchini China, ambayo ni moja ya hospitali za kwanza kuwatibu wagonjwa katika siku za kwanza za mlipuko huo mwishoni mwa mwaka 2019.
Kundi hilo linaloongozwa na WHO, ambalo lililotoka chini ya karantini ya wiki mbili jana Januari 28, 2021, litatembelea maabara, masoko na hospitali katika muda wake uliosalia wa wiki mbili jijini Wuhan ambapo kisa cha kwanza cha corona kiligunduliwa.
Mkuu wa kitengo cha dharura wa WHO, Mike Ryan, amesema kuwa shirika hilo limeamua kufanya utafiti ili kupata majibu ya kina juu ya ugonjwa huo..
Mmoja wa wataalamu wa ujumbe huo wa WHO, Thea Fischer, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba ni muhimu kukumbuka kuwa mafanikio ya kundi hilo na kufuatilia asili ya virusi hivyo vinategemea kikamilifu uwezo wa kufikia vyanzo husika na ushirikiano kutoka kwa serikali ya China.