
KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema kuwa straika mpya wa timu hiyo Junior Lokosa atakiwasha kwenye mchezo ujiao dhidi ya TP Mazembe utakaochezwa Jumapili hii baada ya kukosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Al-Hilal.
Gomes alisema licha ya kuwa mwamba huyo alikuwa kwenye benchi wakati timu yake ikishinda 4-1, alishindwa kumtumia kwa kuwa aliona bado anatakiwa kuwatazama wenzake wanafanya nini ili ajue nini kinatakiwa kwenye timu hiyo, hivyo katika mchezo ujao atakuwa wa kwanza kumuweka kikosini.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Gomes alisema Lokosa hakupata muda wa kucheza kwa kuwa alichelewa kidogo kujiunga na kikosi hivyo alitakiwa kupata muda kidogo wa kujiandaa kwa siku mbili zaidi na kuwatazama wenzake, kwa sasa yupo tayari kucheza mchezo ujao dhidi ya TP Mazembe na ataanza kwenye kikosi cha kwanza.

“Lokosa nilimjumuisha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Al-Hilal lakini sikupanga kumtumia kwa sababu hakuwa tayari kwa mchezo kama unavyojua alichelewa kidogo kuingia kambini.
Lakini mchezo wa TP Mazembe lazima atacheza kwa sababu ya ni mashindano yao na ni nafasi kwake kuonyesha ubora wake,” alisema Gomes.
Simba, keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa watatupa karata yao ya mwisho kwenye michuano ya Simba Super Cup dhidi ya TP Mazembe, wakati leo Ijumaa, Mazembe watacheza dhidi ya Al-Hilal saa 11:00 jioni hapohapo kwa Mkapa.
Stori na Issa Liponda, Dar es Salaam