
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amemweleza Rais John Magufuli kuwa vipo viporo vyote alivyoahidi mwaka 2015 na 2020, wakati akizindua Bunge, ukiwemo ukamilishaji wa katiba mpya, ambapo amemuomba aukamilishe kwani yeye na Makamu wa Rais walikuwa wajumbe wa Bunge la Katiba.
Lipumba amefikisha suala la katiba mpya mbele ya Magufuli leo Jumatatu, Februari 1, 2021, Jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya kilele cha wiki ya sheria.
“Nikialikwa na majaji lazima nifike, mahakama inaponialika Siku ya Sheria najitahidi kuja kwa sababu IGP Sirro anaweza kukupeleka huko, wakiwa wanakuonaona wanajua huyu mtu wetu, Rais Magufuli nakushukuru kwa kunipa fursa ya kutoa pongezi kwa miaka 100 ya Mahakama Kuu.
“Rais Magufuli kwenye hotuba yako ulipokuwa unazindua Bunge Novemba 13, 2020 uliwaeleza wabunge wazingatie uliyoeleza kwenye hotuba yako ya Novemba 20, 2015, ulisema utahakikisha uliyoahidi 2015 yote yanatekelezwa, ulisema kuna kiporo cha kukamilisha Katiba Mpya. Nina uhakika jambo hili utalishughulikia na utatuachia urithi wa katiba inayotokana na maoni ya wananchi.
“Ulipokuwa unapokea ripoti ya Tume ya Uchaguzi 2016 ulisema masuala ambayo yamo ndani ya Katiba iliyopendekezwa na kama kuna watu wana maoni mengine Serikali yako ipo wazi itapokea, nashukuru kwa kusema viporo vyote katika miaka hii mitano utavitekeleza.
“Mhe. Rais nakuombea kwa moyo wa dhati Mungu akupe nguvu, hivi viporo uvitekeleze ikiwemo kuwa na Katiba inayotokana na mapendekezo ya Wananchi wa Tanzania, na kwa bahati sana wewe mwenyewe ulikuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
“Tunatoa wito kwa Rais Magufuli Agenda ya kupata Katiba mpya yenye misingi ya Demokrasia na kumaliza mchakato wa kupata katiba inayotokana na maoni ya Wananchi wa Tanzania , tupo tayari utunyan’ganye Agenda hii iwe Agenda yako,” amesema Prof. Ibrahim Lipumba.
CUF jana kimezindua Kongamano la kudai Katiba mpya na Tume huru ya Uchaguzi, ikiwa ni siku 53 baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania kufanyika ambapo Prof. Lipumba alitoa rai kwa Rais John Magufuli kuheshimu maoni ya wananchi kwa kuwapatia Katiba mpya na Tume Huru.
Vilevile, alisema Rais anatakiwa kuheshimu ukomo wa Uongozi uliopo kwa mujibu wa Katiba na kuepuka majaribio yoyote ya kumwezesha kukaa madarakani kwa muda mrefu.
Alisema Rais anapaswa kufufua mchakato ya kuandika Katiba mpya kuwapatia Watanzania Tume huru ya Uchaguzi itakayounganisha Taifa na kufuta machungu yaliyotokana na Uchaguzi Mkuu wa 2020 na kwamba rasimu ya Katiba mpya iliyo chini ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba imekidhi matakwa ya wananchi walio wengi na jukumu alilobaki nalo Rais ni kuhitimisha mchakato huo.