
KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes Da Rosa, amesema anaamini kikosi chake kitaibuka na ushindi Katika michezo yao miwili ya viporo iliyobaki na kuweza kuwashusha Yanga kutoka kileleni mwa msimamo wa ligi.
Simba, juzi Alhamisi ilianza vizuri kampeni yake ya kutafuna viporo vyao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya kikosi cha Dodoma Jiji, mabao ya Simba katika mchezo huo yaliwekwa kambani na mshambuliaji, Meddie Kagere na Benard Morrison.
Ushindi huo umeifanya Simba sasa kufikisha pointi 38 katika michezo yao 16 waliyocheza mpaka sasa na kuwafanya wawe nyuma kwa pointi sita pekee dhidi ya viongozi wa msimamo klabu ya Yanga wenye pointi 44 huku Simba wakiwa na michezo miwili mkononi ambayo ni dhidi ya Azam FC na Namungo FC.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa Gomes katika michuano ya ligi huku ukiwa ni wa tatu kwa Mfaransa huyo ambaye tayari ameiongoza Simba katika michezo mitatu, miwili ya Simba Super Cup na mmoja wa ligi akishinda mechi mbili na kutoa sare mchezo mmoja.
Akizungumza na Championi Jumamosi,Gomes alisema: “Tumefanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Dodoma Jiji, nikiri kuwa ulikuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa wapinzani.“Changamoto za miundombinu ya uwanja, lakini jambo zuri ni kwamba tumefanikiwa kupata tulichokifuata.“

Tumesaliwa na michezo miwili ya viporo kwenye ligi ambayo ni sawa na pointi sita, malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda michezo hiyo na kuwashusha Yanga kutoka kileleni mwa msimamo licha ya kwamba tunajua haitakuwa kazi rahisi kutokana na ratiba yetu kutubana.”
Said Ally na Joel Thomas, Dar es Salaam