×

Bayern Mabingwa wa Dunia

Timu ya Bayern Munich ya Ujerumani, usiku wa jana ilitwaa Kombe la Dunia kwa vilabu kwa kuwafunga timu ya Tigres UANL toka Mexico kwa bao 1-0.

 

 

Goli lililowapa ubingwa lilifungwa na mlinzi Benjamin Pavard katika dakika ya 59 ya mchezo, kufuatia pasi ya mshambuliaji wao ‘mahiri’ wa timu hiyo Robert Lewandowski, huku timu ya Tigres ikipambana kusawazisha bila mafanikio.

 

 

Michuano hii iliyoshirikisha timu 6 kutoka mashirikisho ya mabara 5 tofauti, ikiwemo CAF, UEFA, CONMEBOL, CONCACAF, AFC na OFC iliyoanza tarehe 1/02/2021 hadi 11/02/2021, ilishuhudia Bayern wakiibuka mabingwa baada ya kipenga cha mwisho katika uwanja wa Education City nchini Qatar.

 

 

Bayern alitarajiwa kuwa mabingwa wa mashindano haya kutokana na ubora wa kikosi chao, ukifananisha na vikosi vya washiriki wengine, huku historia ikionesha kwamba wawakilishi kutoka bara la Ulaya ( UEFA), huwa na nguvu sana kwenye mashindano haya.

 

 

Pamoja na historia hiyo bado ni ukweli usiopingika kwamba kwa sasa kwa Ulaya Bayern ndiyo timu bora, kutokana na mafanikio inayoyapata chini ya kocha Hans Flick, hili likiwa ni kombe lake la 6 yakiwemo ya kitaifa na kimataifa.

 

 

Bayern ameyafikia mafanikio aliyoyapata Barcelona mwaka 2009 chini ya kocha Pep Guardiola kwa kutwaa vikombe tofauti 6 ndani ya msimu mmoja wa kimashindano na kufanya kuwa vilabu viwili pekee Duniani kufanya hivyo.

 

 

Wawakilishi wa Africa Al Ahly ya Misri walimaliza katika nafasi ya 3 na kutwaa medali ya shaba baada kupata ushindi wa penati 3-2, dhidi ya Palmeiras kutoka Brazil baada ya kwenda suluhu ya 0-0 katika dk 90 za kawaida.

 

Leave a Comment