×

Kaze Ajivisha Mabomu, Atupa Kombora Simba

BAADA ya mchezo wa Dar es Salaam Dabi kusogezwa mbele, Kocha Mkuu wa Yanga Mrundi Cedric Kaze ameibuka na kutamka kuwa ni nafasi nzuri kwao kujipanga kuhakikisha wanafunga wapinzani wao Simba.

 

Awali, mchezo huo ulipangwa upigwe Februari 20, mwaka huu kabla ya juzi Bodi ya Ligi Kuu Bara kutangaza kusogeza mbele hadi Mei 8, mwaka huu.

 

Bodi ya ligi imesogeza mbele mchezo huo ili kuipisha Simba inayoshiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo leo Ijumaa itavaana na AS Vita ya DR Congo.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Kaze alisema kubadilishwa kwa ratiba, kwao siyo tatizo na hakuwavurugii mipango yao ya ushindi mara watakapokutana na Simba tarehe hiyo iliyopangwa na Bodi ya Ligi.

 

Kaze alisema kuwa hivi sasa maandalizi yake ameyaelekeza mchezo dhidi ya Mbeya City watakaocheza keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

 

Aliongeza kuwa maandalizi anayoyafanya ya kikosi chake siyo kwa ajili ya timu moja pekee ya Simba bali kwa kila timu atakayokutana nayo katika ligi na Kombe la FA.“Kiukweli kubadilishwa kwa ratiba hiyo kwetu siyo tatizo, kwani wahusika wanaosimama ligi ndiyo wamepanga hivyo, basi tunajipanga kwa ajili ya michezo ijayo ya ligi.

 

“Na mchezo unafuatia wa ligi tunacheza dhidi ya Mbeya City, tupo katika maandalizi hivi sasa ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri na hicho ndiyo kitu tunachokiangalia.“

 

Tukiendelea na michezo hiyo ya ligi tunajua tutakutana na Simba hiyo Mei 8, tunajipanga kuona tukikutana nao tunawafunga“Kama benchi la ufundi sisi kwetu tunazipa umuhimu mkubwa mechi zote kwani zote ngumu zenye ushindani mkubwa, lakini ugumu huo hautafanya tuogope, zaidi tunajipanga kupata ushindi,” alisema Kaze.

Stori: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave a Comment