
HAYAWI hayawi, sasa ni rasmi yamekuwa! Ndivyo kilivyoanza kunyetisha chanzo chetu cha uhakika juu ya kufungwa kwa ndoa ya Malkia wa Bongo Movies, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mchumba’ke wa kitambo ambaye ni na Mkurugenzi wa Radio E-FM na TVE, Francis Shiza ‘DJ Majizo’.
PETE ZAIDI YA MIAKA MITATU
Baada ya kuvishwa pete ya uchumba na kukaa nayo kwa zaidi ya miaka mitatu tangu alipovishwa mwaka 2018 huku baadhi ya mashabiki wake wakimponda kila kukicha kuwa anatakiwa aolewe sasa, hatimaye ndoa ya Lulu anayetikisa kwenye kiwanda cha filamu za Kibongo, sasa muda wa ndoa umefika.
Hata hivyo, kutokana na maoni ya mashabiki hao, Lulu amekuwa akijikuta akipaniki na kuwajibu vibaya kiasi cha kuibua mjadala na mashambulizi makali.
MTU WA KARIBU AMWAGA UPUPU
Akizungumza na gazeti hili la Risasi Jumamosi kwa sharti la kutotajwa gazetini, mtu wa karibu wa familia hiyo ya Lulu ambaye ameomba hifadhi ya jina anasema kuwa, ndoa ipo kama kawaida hivyo watu wakae mkao wa kula tu.
“Wanaosema sana juu ya ndoa ya Lulu na Majizo kubuma, wanajidanganya kwa sababu ndoa ipo kama kawaida.
“Tena hivi ninavyokwambia hapa, wote wawili; yaani Lulu na mchumba wake wapo bize kwelikweli kuhangaikia hilo suala ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.
“Siku chache tu zilizopita walikuwa kanisani (Kanisa Katoliki la Mbezi-Beach jijini Dar).“
Walikwenda kujiandikisha kwa ajili ya kuandaa mazingira ya ndoa yao na wao wenyewe wamesema kuwa, ndoa yao wanataka iwe ya kawaida sana hivyo huwenda kusiwe na zile shamrashamra ambazo watu wanazitegemea.
“Ndiyo! Wamesema wanataka kufunga ndoa ya kawaida mno, tofauti na watu wanavyofikiria.
“Pia inawezekana wasiende kufungia kwenye kanisa hilo walilojiandikisha kwa kukwepa mashuhuda wengi ambao wameshajua ndoa itafungwa kanisani hapo,” anasema mtoa upupu huo ambao ndiyo habari ya mjini kwa sasa na kuongeza;
“Kwa sasa kinachoendelea ni maandalizi kabambe nyumbani kwa Mama Lulu (Lucresia Karugila, maeneo ya Mbweni jijini Dar).”

ILIBUMA?
Matangazo ya kufungwa kwa ndoa ya Lulu na Majizo yalianza kusikika katika Kanisa Katoliki la Mbezi-Beach jijini Dar, mwezi Oktoba, mwaka jana.Kwa mujibu wa matangazo hayo, ndoa ya Lulu na Majizo ilipangwa kufungwa Novemba 2, mwaka jana, lakini ghafla kukaibuka sintofahamu.
Baada ya hapo kumekuwa na fukuto la jambo hilo kutotimia kwa matarajio hayo ya mashabiki wengi wa Lulu.
Hata hivyo, kila mara Lulu amekuwa akitoa majibu tata juu ya kutofungwa kwa mara nyingine.“Tuipe mitano tena,” Lulu alimjibu mmoja wa mashabiki wake kwenye Mtandao wa Instagram.Kabla ya matangazo ya ndoa hiyo kanisani, vuguvugu la ndoa hiyo liliibuliwa na Majizo ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram, alitupia picha akiwa na Lulu na kuandika; “Comments zihusu ukumbi gani utatosha!
”SASA NI KABLA YA KWARESMA
Hata hivyo, baada ya kutangazwa kanisani, matumaini ya wengi yalifufuliwa, lakini ilibuma, lakini sasa ni rasmi kabla ya Mfungo wa Mwezi wa Kwaresma kwa Wakristo ambao unatajwa kuanza wiki ijayo.
TULIKOTOKA
Lulu na Majizo wamekuwa wakijiiba kimapenzi kwa muda mrefu, ambapo Septemba 2018, uchumba wao uliingia kwenye hatua ya kuvishana pete ya uchumba kisha wakatulia zao.Tangu hapo, hawaoani… hawaoanizikawa nyingi hadi kufikia hatua ya uzushi kuenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba, Majizo ameamua kubadili gia angani na kuachana na Lulu.
Mara nyingi wawili hao, wamekuwa kama wanacheza na akili za watu, kwa kuacha kila lisemwalo juu yao mitandaoni na kwenye vyombo vya habari lipite bila majibu yao kuhusu ndoa yao.
Kabla ya Lulu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Majizo, alikuwa akitoka na aliyekuwa kinara wa filamu za Kibongo, marehemu Steven Kanumba, ambaye baadaye aliingia matatani kwa kuhusika na kifo chake.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 kwa kile kinachotajwa kuwa, ni baada ya kutokea ugomvi wa kimapenzi kati yake na Lulu, ambaye alikwenda nyumbani kwa Kanumba usiku wa tukio hilo.
Kufuatia kifo cha Kanumba, Lulu aliingia kwenye msukosuko wa kisheria, hadi Novemba 2017 alipokutwa na hatia ya kuua bila kukusudia na mahakama kumfunga jela miaka miwili. Hata hivyo, Mei 12, 2018, staa huyo alitoka jela na kutakiwa kumalizia kifungo chake kwa kufanya kazi za kijamii kwa amri ya Mahakama Kuu.
Kufuatia mauaji hayo ya kutokusudia ya Kanumba, Lulu alijikuta kwenye mgogoro na mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa.Mara kadhaa mama Kanumba amenukuliwa akimlaani Lulu, kwa kile alichokuwa akikitaja kuwa ni kuhusika kwake na kifo cha mwanaye na baadaye kujitenga naye.
STORI: MEMORISE RICHARD, DAR