UNYANYAPAA na ubaguzi umetajwa kuwa chanzo kikubwa kinachochangia uwepo wa maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI kutokana na Jamii kuhofia kutengwa na wengine kuacha kufuatilia huduma za matibabu.
Akizungumza Julai 15, Wilayani Bagamoyo katika mafunzo yaliyohusisha wataalam,waratibu wa UKIMWI na viongozi wa kijamii kutoka Mkoa wa Dar es Salaam ,Mshauri Mwandamizi wa Afya ya Jamii Dokta Katanta Simwanza amesema Jamii inapaswa kuachana na dhana hiyo ili dhamira ya serikali na wadau katika mapambano ya Virusi vya UKIMWI iweze kufanikiwa.
“Kwa nini tunahamasisha Jamii iachane na Unyanyapaa,ni kwamba hata upande wa vijana hasa wakike tunaona mwitikio wa kwenda kupata huduma za afya ni mdogo,na hii ni kutokana na kuogopa maswali mengi ya namna alivyopata maambukizi,imani iliyopo kuwa wanaopata maambukizi wamepata kwa njia ya kujamiiana ilhali vijana wengi unakuta maambukizi amezaliwa nayo,”alisema.
Akielezea madhara ya unyanyapaa na ubaguzi katika Jamii,Mratibu wa Programu za UKIMWI na Jinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uwezeshaji wa wanawake (Un Women), Jacob Kayombo amesema husababisha wengine kupoteza ajira,riziki,Mali,marafiki na uhusiano.
“Ili kuondokana na Unyanyapaa na ubaguzi kwa watu waoishi na VVU ni muhimu kutambua vichocheo vya mila hatarishi,Unyanyapaa na ubaguzi lakini pia kuishawishi serikali na wadau juu ya matumizi ya sera,Sheria,kanuni na miongozo Ili kupunguza mila hatarishi,Unyanyapaa na ubaguzi unaohusiana na VVU,”alisema.
Mafunzo hayo yanatolewa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Nchini (TACAIDS) kwa kushirikiana na Shirika la Un Women kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Global (Global Fund).


