
KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes, amefunguka kuwa hesabu zake ni kuhakikisha kwamba anapata pointi zote tisa katika mechi zao za nyumbani za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo ameongeza kuwa tayari ameshaweka mikakati ya kupata pointi hizo kwa kuwapa majukumu nyota wake ikiwemo wa eneo la ulinzi.
Mfaransa huyo ataiongoza Simba kupambana na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar Februari 23.
Mchezo huo unafuata baada ya ule wa awali Simba kuishangaza Afrika kwa kushinda ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya AS Vita nchini DR Congo.
Gomes ameliambia Championi Jumatatu, kuwa hesabu zake ni kutwaa pointi hizo za nyumbani ambazo kwa kiasi kikubwa zitawasaidia katika kusonga mbele kwenye hatua ya robo fainali.
“Kitu cha kwanza ni kuwa tumemaliza mechi yetu ya kwanza na tukapata ushindi ambao ulikuwa muhimu kwetu.
“Sasa tunaweka mipango ya kupata pointi kwenye mechi zetu za hapa nyumbani ambazo ni muhimu sana.
“Tayari tumeshaona baadhi ya makosa ambayo tutayafanyia kazi hasa kwenye eneo la ulinzi ambalo ni muhimu zaidi,” alimaliza Mfaransa huyo.
SAID ALLY, Dar es Salaam.