×

Watumishi wa Serikali Kizimbani kwa Tuhuma za Wizi

Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Songwe leo tarehe 15/02/2021 imewafikisha watumishi wa umma wawili(02) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Songwe.

 

 

Watumishi hao wanatuhumiwa kwa nyakati tofauti kutenda makosa ya Wizi wakiwa Watumishi wa Umma kinyume na kifungu cha 270 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 ya Mwaka 2019.

 

 

Mtumishi Jenson Jelas Shitindi (miaka 48) amefunguliwa kesi ya Jinai Na.32/2021 katika mahakama hiyo Mbele ya Hakimu Mkazi, Mh. Vitalis Changwe.

 

 

Akimsomea shtaka linalomkabili, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Mkoa wa Songwe, Bw. Emanuel Ndembeka alisema kwamba mshtakiwa kwa tarehe tofauti kati ya m waka 2015 na mwaka 2020 akiwa katika Kijiji cha Mlangali, Mbozi Mkoani Songwe, kwa nia ovu na pasipokuwa na uhalali wowote.

 

 

Akiwa ni Mwajiriwa wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi kwa wadhfa wa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mlangali, aliiba fedha kiasi cha Shs.2,451,096/= ambayo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi. Fedha hiyo ilitokana na makusanyo yaliyofanywa kwa njia ya mfumo wa kielektroniki maarufu ikijulikana kwa jina la POS.

 

 

Mshtakiwa alikana shtaka na kisha kuamriwa kwenda mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana. Upelelezi wa kesi umekamilika na kesi husika imeahirishwa mpaka tarehe 02/03/2021 itakapotajwa kwa ajili ya usikilizwaji.

 

 

Mtumishi Shadrack Joseph Mgallah (miaka 47) amefunguliwa kesi ya Jinai Na. 33/2021 katika mahakama hiyo Mbele ya Hakimu Mkazi Mh.Vitalis Changwe.

 

 

Akimsomea shtaka linalomkabili, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Mkoa wa Songwe Bi. Simona Mapunda alisema kwamba mshtakiwa kwa tarehe tofauti kati ya m waka 2017 na mwaka 2020 akiwa katika Kijiji cha Hatelele kilichopo wilayani Mbozi Mkoani Songwe.

 

 

Kwa nia ovu na pasipokuwa na uhalali wowote, akiwa ni Mwajiriwa wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi kwa wadhfa wa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Hatelele, aliiba fedha kiasi cha Sh 7,981,986.10/= ambayo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi. Fedha hiyo ilitokana na makusanyo yaliyofanywa kwa njia ya mfumo wa kielektroniki maarufu kwa jina la POS.

 

 

Mshtakiwa alikana shtaka na kisha kuamriwa kwenda mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana. Upelelezi wa kesi umekamilika na kesi husika imeahirishwa mpaka tarehe 03/03/2021 itakapotajwa kwa ajili ya usikilizwaji.

 

NA Dicksoni Kapungu SONGWE
Tarehe 15/02/2021

Leave a Comment