
OFISA Mauzo wa Kampuni ya Amsons Industries Tanzania Limited, John Joseph (40), mkazi wa Kimara Michungwani jijini Dar es Salaam amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kufanya wizi wa zaidi ya sh. milioni 89 akiwa mwajiriwa wa kampuni hiyo.
Akisomewa hati ya mashtaka na wakili wa serikali, Kija Luzungana, amesema mshtakiwa anakabiliwa kosa moja la kufanya wizi wa zaidi fedha hizo mil. 89 kupitia bidhaa alizokuwa amekabidhiwa na mwajiri wake ambalo kosa hilo anadaiwa kulitenda Aprili 20, 2017 na 2018 katika wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam. Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo.
Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Rashid Chaungu, amesema dhamana kwa mshtakiwa ipo wazi na anatakiwa kuwa na fedha taslimu nusu ya kiasi anachotuhumiwa ambacho ni mil. 40 au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya mil. 22 kila mmoja pamoja na barua za utambulisho wao vikiwemo vitambulisho vya taifa.
Aidha hakimu amesema endapo mshtakiwa atatimiza masharti ya dhamana hatotakiwa kusafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kuwa na barua ya mahakama au kibali cha mahakama.
Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti hayo na amepelekwa rumande, hivyo kesi imeahirishwa hadi Machi Mosi mwaka huu.