×

Kachero Adai Alikataa Hongo Kesi Dawa za Kulevya

 

SHAHIDI wa tano wa upande wa mashtaka katika kesi ya ulimaji wa dawa za kulevya aina ya bangi na kufanya mauzo ndani na nje ya nchi, inayomkabili mwekezaji wa kigeni, amedai kuwa mshtakiwa huyo alimwomba wamalizane kimyakimya kwa dau la Sh. milioni 10.

 

 

Kesi hiyo inamkabili raia huyo wa kigeni, Damian Jankowski na wenzake watatu, na kuwa mshtakiwa huyo alimwahidi shahidi huku akiahidi kumlipa pesa kila mwezi.

 

 

Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2020, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Bernazitha Maziku, inawakabili Jankowski raia wa Poland na wastakiwa wenzake Eliwaza Pyuza, Hanif Kanani na Boniface Kessy.

 

 

Akiongozwa kutoa ushahidi wake jana mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Verdiana Mlenza, Mkaguzi wa Polisi, Inspekta Hassan Msangi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), alidai wakati anafanya upekuzi nyumbani kwa Jankowski, mfanyabiashara huyo alimuita pembeni na kumweleza kwamba yuko tayari kumlipa Sh. milioni tano ili aachane naye.

 

 

Baada ya kuona ofisa huyo wa polisi hayuko tayari, alipanda dau na kumwambia atampa Sh. milioni 10 na vilevile kila mwisho wa mwezi awe anaenda kwake kuchukua pesa, lakini alikataa na kumwambia binafsi yuko kazini na hawezi kuhitaji hivyo vitu.

 

 

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa na Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka akisaidiana na Verdiana Mlenza, wakati mshtakiwa wa kwanza, wa pili na watatu katika kesi hiyo, wanatetewa na Wakili FayGrace Sadala. Kesi hiyo itaendelea tena leo.

Leave a Comment