×

Rais Magufuli Ampa Siku 7 Waziri Simbachawene – Video

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, amempa siku saba Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene, ahakikishe wastaafu wote wa jeshi la polisi wanaodai mafao yao wanalipwa ndani ya siku hizo.

 

Rais Dkt. Magufuli ametoa maagizo hayo Februari 26, 2021, wakati akizungumza na Askari Polisi mara baada ya kuzindua Chuo cha Maafisa wa Polisi Kurasini Dar es Salaam, ambapo awali IGP Sirro alimuomba Rais Magufuli awasaidie wastaafu ambao hawajalipwa mafao yao waweze kulipwa kwa wakati.

 

 

“Kuna suala la wastaafu wa jeshi la polisi kutokulipwa mafao yao, mimi nawashangaa Wizara ya Mambo ya Ndani una mstaafu wako amefanya kazi nzuri na amemaliza bila tatizo lolote anatakiwa kulipwa mafao yake Waziri unakaa bila kwenda kuwaombea.

 

“Kwa nini usichukue haya majina ukaenda Wizara ya Fedha ukasema nina wastaafu nataka pesa zao, tatizo Mawaziri wangu hamuwasiliana mnafanya watu wa chini kupata shida, huu ni wajibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani nikificha nitakuwa mnafiki.

 

“Mimi wakati nikiwa Waziri wa Ujenzi tunapopata shida ya makandarasi nilikuwa naenda kufanya fujo mpaka pale Wizara ya Ujenzi na wala hawakunipenda naenda Wizara ya Fedha nataka fedha ya makandarasi na walikuwa wanalipwa.

 

“Wizara ya Mambo ya Ndani nawashangaa, una Mstaafu amemaliza Polisi bila shida anatakiwa kulipwa mafao, Waziri, Katibu Mkuu mmekaa tu bila kwenda kuwaombea!, kwanini msipeleke majina Wizara ya Fedha? Tatizo Mawaziri wangu hamuwasiliani, mnawapa shida Watu wa chini.

 

 

“Wenye Wizara ya Mambo ya Ndani Wastaafu wenu wanamaliza kazi wala hamuendi kugombana na Wizara zinazohusika wakalipwe hela? Kwa hiyo na IGP siku ukistaafu Simbachawene hatoshughulikia malipo yako, hilo ulijue, hili ni tatizo la wakubwa wenu Wizarani.

 

 

“Haiwezekani Wastaafu wa Polisi mpaka wamsubiri Rais akashughulike nao, mbona Jeshini wakistaafu hawanisubiri Mimi? Niwaombe Wastaafu muwalaumu Simbachawene, Naibu Wake, Katibu Mkuu wake, Naibu Katibu Mkuu wake na Wakurugenzi, mumuunganishe na IGP kwa sababu hapigi kelele.

 

 

“Hawa viongozi wenu wakitaka Wastaafu walipwe watalipwa wala haiwezi kuchukua siku tano, watu wamekuwa Maofisa, wana manyota, wamefanya kazi kubwa wamekoswakoswa marisasi na majambazi, anastaafu mnashindwa kumlipa, it’s not fair, hii ni challenge kwenu viongozi wa Wizara.”
 

“Waziri Simbachawene nakuagiza nenda kashughulikie malipo ya wastaafu na ikiwezekana ndani ya wiki moja wawe wamelipwa, tuliwatumia vizuri wakati hawajastaafu ni lazima wafaidike na kustaafu kwao hakuna kinachoshindikana pesa ipo,” amesema Rais Dkt. Magufuli.

Leave a Comment