
Leo September 13 Jijini Dodoma, Rais Samia ameagiza Wakuu wa Mikoa kuanza kuwapanga upya wafanyabishara wadogo maarufu kwa jina la Machinga. Rais Samia amesema Machinga wamekua wakizuia maduka ya watu na kupelekea serikali kupoteza kodi.
Ameyasema hayo wakati akiwaapisha Mawaziri wapya walioteuliwa mwishoni mwa wiki. Mawaziri walioapishwa ni January Makamba (Waziri wa Nishati), Dr. Asha Kijatu (Wizara ya Habari na Mawasiliano), Prof. Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi) na Dr. Stagomena Tax (Waziri wa Ulinzi).
Rais Samia amewataka Wakuu wa Mikoa kuwapanga kwenye maeneo yatakayoondoa kero kwa watumiaji wa njia pamoja na wamiliki wa maduka ambao hivi karibuni wametoa malalamiko kuwa wanakosa mapato kwasababu biashara wanazofanya zinafanana na za Machinga ambao hawalipi kodi.
“Najua kwamba Serikali tumetoa fursa kubwa kwa machinga kufanya biashara zao ili kujiingizia vipato vyao. Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanawapanga lakini imefika wakati wameenea kila mahali, mpaka kwenye maduka yao wanaziba na wenye maduka hawauzi.
“Wenye maduka nao wanaamua kutoa bidhaa kwenye maduka yao na kuwapa machinga, hili linaikosesha Serikali mapato kwa sababu machinga halipi kodi lakini mwenye duka anatakiwa kulipa kodi.
“Naomba wakuu wamikoa mchukue hatua mapema za kuwapanga machinga, sitaki kuona ninayoyaona kwenye TV, ngumi, kupigana, kuchafuliana, vyakula kumwagwa hii hapana, naomba mchukue hatua vizuri za kuwapanga bila kuudhi wenye maduka wala machinga bila vurugu.
“Nitoe wito kwa machinga na wajitahidi kufuatia sheria zilizowekwa na kufuata yale wanayoelekezwa na wakuu wao wa mikoa. Niwatakie kazi njema mlioapa leo na wale mlioko kazini mkaendeleze kazi, nami nakwenda kendelea na kazi ya marekebisho. Asanteni sana,” amesema Rais Samia.