
Kocha mwingine aliyetajwa kuchukua mikoba hiyo, ni Mbelgiji, Patrick Aussems ambaye aliipa mafanikio Simba ya kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/19, kabla ya kutimuliwa Novemba 2019.
Pia alitwaa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA. Aussems ambaye hivi karibuni alipata dili la kuinoa AFC Leopards ya Kenya, imeonekana maisha ya Kenya yamemshinda na kutaka kurudi Tanzania.
Kaze na benchi lake la ufundi, juzi Jumapili usiku lilivunjwa kutokana na mwendo mbovu wa timu hiyo kwa mujibu wa uongozi.
Hiyo ikiwa ni saa chache tangu Yanga itoke sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, makocha hao ndiyo waliopendekezwa na Kamati ya Utendaji ya Yanga iliyofanya kikao kizito mara baada ya mchezo dhidi ya Polisi Tanzania kumalizika.
Mtoa taarifa huyo alisema Mwambusi na Maxime watakabidhiwa timu hiyo kufundisha kwa ajili ya kumalizia michezo ya ligi ya mzunguko wa pili pekee.

Aliongeza kuwa, mara baada ya msimu kumalizika, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije raia wa Burundi ndiye atakayekuja kuungana na kina Mwambusi kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao wa 2021/2022.
“Mara tu baada ya kutangaza kulivunja benchi la ufundi, haraka uongozi tulikutana kwa ajili ya kujadiliana mipango mipya ya timu na kikubwa katika kupendekeza jina la kocha wetu mpya mkuu atakayekuwa na msaidizi wake.
“Kati ya majina tuliyoyapendekeza ni Mwambusi atakayekuwa kocha mkuu na msaidizi wake ni Maxime ambao watamalizia msimu huu katika michezo iliyosalia.
“Baada ya msimu tutamtangaza kocha wetu mpya, tayari tunayo majina ya makocha hayo na anayepewa nafasi kubwa hadi hivi sasa ni Ndayiragije,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
“Pia kuna taarifa za Kocha Aussems kuwa njiani kuja kuifundisha Yanga.”Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kuzungumzia hilo, alisema:
“Hilo suala lipo kwa uongozi, hivi karibuni kocha mkuu mpya atakayekuwa na msaidizi wake watatangazwa, hivyo tupeni muda kidogo.”Katika hatua, Kaze baada ya kuvunjiwa mkataba wake, alisema:
“Nimefurahi kufanya kazi na Wananchi kwa muda wa miezi mitano niliyoitumikia kwa pamoja.
“Katika kipindi hicho chote tumepata furaha na tukapata wakati mugumu lakini niseme kuwa ni mambo ya mpira, subira ilikuwa ngumu kwa mashabiki wengi wa Yanga.
“Ninaondoka Yanga nikiwa kifua mbele kwa kuwapa Kombe la Mapinduzi, ninaamini walipata furaha kubwa, hivyo niwatakie kila la kheri katika mbio zao za ubingwa wa ligi msimu huu.
”Kaze kwa kipindi cha miezi mitano akiwa Yanga, aliiongoza timu hiyo kucheza mechi 18 za ligi kuu, akishinda 10, sare 7 na kupoteza moja, huku akishinda michezo mitatu kati ya minne ya Kombe la Mapinduzi na kuwa mabingwa.
STORI: WILBERT MOLANDI, Dar