
Licha ya msanii wa Bongo Fleva, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ kumuomba msamaha mwigizaji Kajala Masanja kutokana na tuhuma za kusambaza video chafu za mwanawe Paula Paul ‘Paula Kajala’ mitandaoni, uamuzi huo umebainika kuwa hautapunguza wala kuondoa mashtaka dhidi yake.
Hatua hiyo imekuja ikiwa zimepita wiki chache tangu Rayvanny alipotuhumiwa kutupia picha na video mitandaoni zikimuonesha akiwa na Paula katika mahadhi ya kutomasana kimahaba hali iliyoibua hasira za mama mzazi wa binti huyo, Kajala Masanja aliyeandika waraka mrefu kwenye ukurasa wake wa Instagram huku akimshushia lawama Rayvanny.
Mbali na waraka huo, Kajala ambaye pia ni msanii wa Bongo Movies na mpenzi wa Rajab Abdul ‘Harmonze’ walikwenda kumfungulia mashtaka Rayvanny pamoja na mlimwende Hamisa Mobeto ambaye alidaiwa kushiriki kumkuwadia Paula.

MSAMAHA WENYEWE HUU HAPA
Baada ya kutoka mahabusu kwa dhamana, Machi 5, mwaka huu, Rayvanny aliamua kumuomba Kajala msamaha kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kuandika maneno haya;“Duniani wakati mwingine kuna vitu tunavifanya ambavyo pengine kwa macho yetu ya ujana tunaona ni sahihi, lakini tunasahau upande mwingine wa pili ambao ni wazazi wanaoumia kwa namna moja au nyingine.
“Nichukue nafasi hii kumuomba radhi dada yangu @kajalafrida na kuwaomba radhi wazazi na yoyote ambaye nilimkwaza kwa kuposti video ambayo inawezekana imetafsiriwa vibaya…kwa sababu sisi ni binadamu na kamwe hatuwezi kukamilika.
KAJALA APATA KIGUGUMIZI
Wakati taarifa za msamaha huo zikizidi kusambaa, vyanzo vyetu vimelieleza Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuwa, Kajala bado hajapokea msamaha huo kama ulivyoombwa na msanii huyo.Taarifa zilikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa msamaha huo wa Rayvanny hauwezi kulingana na thamani na mtoto wake kipenzi.“

Kajala hawezi kuonesha wazi ni jinsi gani msamaha huo ameutupilia mbali na umeonekana haukuwa na maana yoyote kwake kwa sababu ameona kama msanii huyo anamkebehi baada ya kuchelea sana kumuomba msamaha,” alisema mpashaji huyo.
Mtoa habari huyo aliendelea kuweka wazi kuwa, inawezekana Kajala ameangalia jambo hilo na kuona wazi kama kuna mchezo mchafu ambao anataka kuchezewa ndiyo maana hajaupokea.
“Ninachokiona hakuna msamaha wa kweli hapo na Kajala anajua wazi kama kuna mchezo ambao siyo mzuri anachezewa,” anasema mpashaji huyo.Baada ya kupata udaku huo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta Kajala ambapo baada ya kuulizwa kuhusu msamaha huo alisema; “Sina cha kuongea kuhusu hilo ila nimeona huo msamaha.
”Kauli hiyo ya Kajala ilidhibitisha kutoukubali msamaha huo hali inayoendelea kumuweka rehani Rayvanny na mwenzake Hamisa.
SHERIA ZINASEMAJE?
Kwa mujibu wa Mwanasheria Joseph Salila, mtuhumiwa kumuomba msamaha mlalamika aliyeshitaki, hakuondoi shitaka dhidi ya mtuhumiwa.
Salila amelieleza Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuwa, suala la msamaha linaweza kuombwa Polisi au mahakamani kwa utaratibu maalum.
“Lakini kwa suala la Rayvanny tunaona kuwa kisheria bado sakata lake ni bichi, hata kama amemuomba Kajala, hilo haliondoi utaratibu wa Polisi kukamilisha upelelezi wa kesi yake na kisha DPP kutolea uamuzi kama kuna kesi au hakuna, kama kuna kesi ya jinai au madai maana mambo ni mengi kwenye sakata lao,” anasema.
Aliongeza kuwa, kama Kajala angeupokea msamaha huo, ina maana kuwa kesi kama itafika mahakamani ingekuwa rahisi kwa Rayvanny kushinda kwa sababu Kajala asingetoa ushirikiano kwenye ushahidi.
“Lakini kama Kajala bado hajaupokea msamaha wake, ina maana kama kesi ikifika mahakamani, Kajala atashirikiana vizuri na upande wa Serikali kutoa ushahidi kisha kufikia hatua ya hukumu,” anasema.
KINACHOCHUNGUZWA NI KIKI
Hivi karibuni, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Japhet Kibona alithibitisha wasanii Hamisa Mobeto na Rayvanny walikuwa wanashikiliwa na Polisi katika Kituo cha Osterbay, lakini waliachiwa kwa dhamana na uchunguzi bado unaendelea kufanyika.
Kamanda Kibona alisema kuwa, kesi hiyo ambayo ni ya Polisi licha ya kwamba hapaswi kueleza walichokizungumza, lakini kilichopo ni kusambaza picha kwenye mtandao bila ridhaa ya mmoja wapo mwenye hizo picha.
“Tunaendelea na uchunguzi kwa kilichofanyika na uchunguzi wetu na upelelezi ndiyo utakaoridhia, pia kuna mwanasheria ambaye atapitia kama kilichofanyika ni kosa la kijinai au la,” alimalizia
Stori; MWandiShi Wetu, Dar