
Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam limeanza kuweka mikakati kwa kushirikiana na jamii kukomesha biashara ya binadamu inayoendelea nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatano Machi 17, 2021 katika uzinduzi wa semina ya mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo maofisa polisi, waendesha mashtaka na mahakimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema moja ya mkakati huo ni kutoa elimu kwa jamii na kuhakikisha matukio yote yanayohusiana na biashara hiyo yanaripotiwa kwa wakati.
“Naamini kupitia mafunzo haya yanaenda kuboresha ufanisi na utendaji kwa kudhibiti matukio hayo, kwanza kuhakikisha matukio yote yanayohusiana na biashara hii yanayoripotiwa kwa wakati na kushughulikiwa kikamilifu na kuhakikisha yasiyoripotiwa yanajulikana ili kukomesha mambo haya yanayopoteza utu wa binadamu.”
“Nategemea elimu itakayotoka hapa itasaidia kuboresha utendaji na kuleta ufanisi kuhakikisha wanakomesha biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu inapungua na kuisha kabisa…, binadamu anaposafirishwa kama bidhaa ni kukiuka haki zilizotamkwa kwenye matamko mbalimbali,” amesema.