
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema baadhi ya wananchi walioshiriki shughuli ya kumuaga Rais John Magufuli wamejeruhiwa baada ya kukanyagwa na wenzao.
Mambosasa ameelezea kuhusu taarifa za kuwepo kwa watu waliojeruhiwa na kukimbizwa hospitali katika shughuli hiyo iliyofanyika Uwanja wa Uhuru na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu.

Kutokana na wingi huo, shughuli ya kuaga ilisitishwa saa 9 alasiri na mwili wa kiongozi huyo ukiwa katika gari maalum ulizungushwa mara tano uwanjani hapo ili maelfu ya wananchi wapate fursa ya kuaga baada ya kuomba kutokana na kuelezwa kuwa wote hawataweza kupita mbele ya jeneza lililokuwa na mwili wa Magufuli.
Katika maelezo yake Mambosasa amesema idadi kamili ya watu waliojeruhiwa katika shughuli hiyo hana lakini ni wengi.

“Binafsi sina idadi lakini ni watu wengi ambao walikanyagana na kukosa hewa. Walikuwa wanaanguka na kubebwa,” amesema Mambosasa. Raia wakiwa wamepanda kwenye uzio ulio kwenye lango kuu la kuingilia uwanjani

Msongamano ulikuwa mkubwa wa watu waliofika kuaga mwili wa hayati Rais John Magufuli huku wengine wakiwa nje wakisubiri kuingia na wengine kukosa uvumilivu licha ya tangazo kutolewa kuwa wote watafanikiwa kutoa heshima kwa kiongozi wao.