
Samia Suluhu Hassan ameandika historia ya kuwa Rais wa sita wa Tanzania akiwa ni mwanamke wa kwanza Tanzania kushika nafasi hiyo kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli. Kulingana na mahojiano aliyofanya kwa nyakati tofauti na vyombo mbalimbali vya habari, kuna ishara mama huyu hakuwahi kufikiria kushika wadhifa aliopata juzi.
Akiwa Makamu wa Rais alikaririwa akisema alikuwa anaamini ipo siku Tanzania inaweza kuwa na Rais mwanamke, lakini hakufikiria mwanamke huyo anaweza kuwa yeye kutokana na ugumu wa kazi hiyo aliouona kwa mtangulizi wake.
“Urais sio jambo jepesi, kwa muda niliofanya kazi kama Makamu wa Rais nafahamu kazi za Rais, nafahamu majukumu mazito aliyonayo, binafsi ukiniambia kuhusu urais lazima nifikirie mara sita sita, sio kwamba siwezi ila najua jukumu ni zito,” alisema Samia katika mahojiano aliyowahi kufanya na TBC.
Akihojiwa na televisheni moja ya mtandaoni (jina tunalo), mama huyu anasimulia safari yake ilianza mwaka 1975 alipohitimu kidato cha nne na kupangiwa kwenda Ofisi Kuu ya Maendeleo visiwani Zanzibar akiwa na umri wa miaka 16.
Kutokana na umri wake kuwa mdogo alirudishwa nyumbani hadi mwaka uliofuata ndipo alipokwenda kuanza kazi rasmi kama Ofisa Masijala, kazi aliyodumu nayo kwa miaka mitatu.
“Nilifanya kazi ile kwa miaka mitatu lakini ilikuwa kama niliowakuta nawaongoza mimi, wakubwa wakitaka kitu wanauliza Samia yuko wapi na kueleza mahitaji yao,” alisema na kuongeza:
“Wenzangu kwenye idara wakawa wanaona kama shawishi (wanajiuliza), inakuwaje kila kitu niulizwe mie, nikahisi hapa nilipo si sahihi nahitaji kuwa mahali pengine,” anasimulia zaidi Samia kwenye video hiyo.
Mawazo hayo inaaminika yalimfanya Samia kuanza kusoma kozi ya takwimu kwa ngazi ya cheti, kisha kozi ya utawala ngazi ya cheti pia, na ili kupandisha sifa zake alikwenda kujiunga na kozi ya astashahada ya uongozi wa umma katika Chuo cha IDM kwa miaka mitatu.
Samia katika mahojiano hayo alisimulia kuwa mwaka 1987 alirejea ofisini kwake na kupanda cheo kuwa ofisa mipango, lakini alikuta mambo yanaenda taratibu kama alivyoacha, jambo ambalo anadai hakulipenda.
Akiwa anaendelea kuitumikia nafasi hiyo ndani ya miaka miwili akaona imetangazwa nafasi ya kazi Shirika la Chakula Duniani (WFP) tawi la Zanzibar, aliomba na kufanikiwa kupata ambapo aliifanya kwa miaka tisa.
“Niliporudi Serikalini ninakona watu wanakwenda `too slow’ (taratibu) nikachomoka nikaenda kwenye asasi za kiraia, nikawa kiongozi wa asasi hizo pale Zanzibar,” alisena na kufafanua:
“Ilikuwa ngumu kwa sababu ilikuwa taasisi changa na hatuna fedha, nikapambana kuongoza hivyo hivyo, ubunifu wangu ukaniwezesha kuandika mradi tukapata fedha mambo yakawa mazuri sasa. Baada ya fedha kupatikana maneno yakaanza nikaona isiwe shida nikaacha,” alisema.
Rasmi kwenye siasa
Baada ya kuachana na asasi za kiraia, Samia akahamishia mawazo yake kwenye siasa, wakati wote huo alikuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) lakini hakuwahi kuwa kiongozi.
Mwaka 2000 akajitosa rasmi katika ulingo wa siasa kwa kuwania viti maalumu kwenye Baraza la Wawakilishi.
“Niliingia kwenye siasa sio kwa matamanio wala utashi. Nilikuwa naona namna wapinzani walivyokuwa na nguvu kwenye Baraza la Wawakilishi, pia mawaziri walikuwa wanajibu ndivyo sivyo, jambo lile lilikuwa linanikereketa.
“Nikasema ngoja na mimi nitaingia huko nikapambane na wapinzani na hawa mawaziri wanaojibu ndivyo sivyo nikawasute, shida ikawa sijui naingiaje,” alisema Samia, ambaye ni mtu wa pili kutoka Zanzibar kupata urais wa Tanzania. Aliuliza na kuelekezwa na kuwania uwakilishi kwa viti maalumu.
Baada ya kupata viti maalumu na kuishia kuwa mjumbe wa baraza, aliteuliwa kuwa waziri katika Serikali, nafasi aliyoitumikia kwa miaka mitano hadi mwaka 2005, aliwania tena viti maalumu na kuteuliwa kuwa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji. Mwaka 2010 akagombea ubunge wa jimbo la Makunduchi.
“Hapo ndipo nilipoona joto ya jiwe, mwanamke nilikuwa peke yangu na jina la kwanza nikapachikwa jina la `kigego’. Nilipofika jimboni nikajifunza mila na desturi, nakumbuka nilikuwa sijifungi ushungi, nikanong’onezwa jitande,” anasimulia Samia.
Samia alipiga kampeni, ambapo alieleza anachotaka kufanya kwenye jimbo hilo na hatimaye akashinda. Baada ya uchaguzi huo aliteuliwa kuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais kushughulikia Muungano.
Mwaka 2014 alichaguliwa kuwa makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba lililoandaa Rasimu ya Katiba Mpya akimsaidia Samuel Sitta.
Haikuchukua muda mrefu nyota yake ikaanza kung’aa na akateuliwa kuwa waziri na rais Amani Karume, akipewa wadhifa wa Waziri wa Leba, Jinsia na Watoto.
Alitumikia taifa hadi mwaka wa 2005 alipochaguliwa tena na kuteuliwa upya kama waziri, wakati huu akipewa wizara ya Utalii, Biashara na Uwekezaji katika serikali ya visiwani.
Mwaka wa 2010 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo la Makunduchi.
Punde tu akateuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa waziri wa maswala ya muungano katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akihudumu chini ya Makamu wa Rais Mohamed Gharib Bilal.
Machi mwaka 2014, aliwania na kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba nmjini Dodoma. Bi Hassan alichaguliwa kwa kura 390 sawa na asilimia 74.6 na kumshinda mpinzani wake Amina Abdalla Amour ambaye alipata kura 126 sawa na 24%.
Julai mwaka 2015, Dkt John Magufuli alimteua kuwa mgombea mwenza lakini baada ya kumaliza mhula wa kwanza, mwaka 2020 alimchagua tena kuwa Mgombea Mwenza na baada ya uchaguzi waliibuka na ushindi hivyo mama Samia akaendelea kuwa makamu wa Rais.
Wale wanaomjua Bi Hassan wanasema kuwa ni mchache wa maneno. Machi 17, 2021 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliaga dunia katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam alipokuwa akipatiwa matibabu, hivyo kwa mujibu wa katiba, Machi 19, Mama Samia aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kazi
Aliajiriwa kama mchapishaji katika serikali ya Zanzibar mwaka 1977 na akapanda ngazi hadi kuwa afisa wa mipango serikalini kati ya 1987 na 1988.
Alihudumu pia kama meneja wa mradi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Zanzibar kati ya 1985 na 1997, na pia kama meneja mkurugenzi wa Mwamvuli wa NGO 1998 hadi 1999.
Bi Samia anasema kuwa njia yake ya ufanisi haijakuwa rahisi kama inavyodhaniwa.
”Safari yangu katika siasa imekuwa njia ndefu na yenye tija.”
Kimsingi ufanisi wangu katika siasa za Tanzania umetokana na uweledi na umakini katika kila jambo ninalolifanya.”
”Sio rahisi kuwajibikia familia yako wakati huohuo ukiendelea na maisha ya siasa elimu na majukumu mengine ya kikazi,” anasema Bi Samia.
Familia
Aliolewa mwaka wa 1978, kwa Bw Hafidh Ameir, ambaye wakati huo alikuwa afisa wa Kilimo .
Walijaliwa watoto wanne.
Mmoja kati ya wanawe Wanu Hafidh Ameir (1982), ni mwakilishi maalum katika bunge la Zanzibar.