
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema zaidi ya watu bilioni 3.9 duniani kote walifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya shughuli ya kitaifa ya kuagwa hayati John Magufuli iliyofanyika kitaifa jana Jumatatu Machi 22, 2021 jijini Dodoma.
Majaliwa ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya mazishi ameyasema hayo leo Jumanne Machi 23, 2021 katika uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar muda mfupi kabla ya viongozi na wananchi kuaga mwili wa kiongozi huyo.
Akivishukuru vyombo vya habari kwa kazi ya kuhabarisha umma nchini na duniani amesema, “nashukuru vyombo vya habari mlikuwa nasi toka siku ya kwanza na mnaendelea kuwahabarisha Watanzania, hata tukio hili mnaendelea kulirusha duniani kote.”
“Mpaka jana jioni tunazo taarifa watu waliofuatilia tukio la kuaga kitaifa jana Dodoma, zaidi ya watu bilioni 3.9 karibu bilioni 4 walikuwa wanafuatilia tukio la kumuaga ile jana” amesema Majaliwa.
Shughuli ya Kitaifa ya kuaga mwili wa Magufuli ilifanyika jana katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Tukio hilo ambalo lilirushwa moja kwa moja na vyombo mbalimbali vya habari kikiwemo Mwananchi Digital lilihudhuriwa na marais tisa. Mwili wa Magufuli leo unaagwa katika uwanja wa Amaan Zanzibar na utalala katika Ikulu ya Zanzibar.