
Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kukejeli kifo cha Hayati Dkt. John Magufuli kwa kupika supu.
Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Urlich Matei amesema ni jambo la kushangaza kwa baadhi ya watu kufanya vitendo hivyo huku nchi ikiwa kwenye maombolezo ya siku 21.
‘’Nchi yetu ipo katika huzuni kubwa ya kuondokewa na mpendwa wetu, Dkt John Magufuli, kufuatia kifo hicho,tupo katika maombolezo kwa siku 21, lakini katika kipindi hiki, polisi mkoani Mbeya tarehe 20 tulipata taarifa ya kuwepo kwa watu wanne wakifanyia kejeli msiba huu’’. Kamanda Matei aliviambia vyombo vya habari jijini Mbeya.
Watu watatu walikamatwa katika eneo la Mwanjelwa wakiwa wameandaa supu ya Mbuzi na utumbo pia wakiwa na ndoo ya pombe ya kienyeji aina ya ulanzi.
‘’Vitendo vile ni ishara ya kuleta tafrani na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo lile’’. Kole Mwasongwe, Asifiwe Mwasaga na Ernest Kaponela walikamatwa wakiwa na supu walioiandaa barabarani eneo la njiani sambamba na pombe.
‘’Tumewachukua na tunaendelea na mahojiano, ushahidi utakapokamilika tutawafikisha mahakamani” alieleza kamanda Matei.
Katika tukio jingine, majira ya usiku wa tarehe 20, eneo la Soweto mtaa wa mabuchani, mtu mmoja kwa jina Tumaini Talazwa alikamatwa kwa kosa la kutoa lugha ya kejeli kuhusu msiba huu. Kamanda wa polisi amewataka wakazi wa Mbeya kutii sheria bila shuruti wakati huu wa maombolezo.