
TAIFA la Tanzania bado lipo kwenye maombelezo ya siku 21 kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais, Hayati John Pombe Joseph Magufuli.
Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Dar alikokuwa akitibiwa matatizo ya moyo.
Rais Samia Suluhu Hassan ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais, ndiye aliyetangaza taarifa za kifo chake na siku 21 za maombolezo.
Baada ya Mama Samia kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taratibu za kumuaga Hayati Dk John Pombe Magufuli zilifanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na hatimaye Geita.
Jana ndiyo mwili wa Hayati Magufuli ulipumzishwa nyumbani kwake Chato mkaoni Geita. Lakini wakati zoezi hilo likihitimishwa jana, nyuma yake kuna maajabu ya Namba 5 katika maisha yake. Katika maajabu hayo ya namba tano, inaelezwa kuwa, Hayati Magufuli hakuyajua au aliyajua na kuyaishi.
KUTWAA URAIS
Mwaka 2015, Hayati Magufuli ndipo alipotwaa kijiti cha urais nchini Tanzania akikalia kiti hicho baada ya awamu ya kwanza iliyoongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere, awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa na awamu ya nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete.
AWAMU YA TANO
Awamu ya 5 ndiyo iliyomtambulisha katika uongozi wake wa nchi. Lakini pia, Hayati Magufuli ndiye alipewa slogan ya mitano tena baada ya kuongoza vizuri miaka mitano ya awali, Watanzania walimtaka aongoze miaka mitano tena.
KULA KIAPO
Novemba 5, mwaka 2015, Hayati Magufuli aliapa katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Novemba hiyo hiyo 5, mwaka 2020 aliapa tena kukamilisha ngwe ya pili ya uongozi wake jijini Dodoma.
MIRADI MITANO
Miradi mitano mikubwa kabisa ndiyo iliyompaisha kitaifa na kimataifa. Miradi hiyo ni; Mradi wa Umeme wa Stigler George (Pwani), Reli ya Kisasa, Standard Gage (SGR), Kuhamishia Serikali Dodoma Makao Makuu ya Tanzania, Kununua ndege 11 kwa fedha za ndani, Kujenga madaraja mawili ya juu mkoani Dar es Salaam (Daraja la Kijazi, Ubungo na Daraja la Mfugale, Tazara).
JUMATANO KIFO CHATANGAZWA
Siku ya Jumatano ndipo Taifa la Tanzania lilipotangaziwa kifo chake na mikoa mitano ndiyo iliyotajwa na serikali kwamba, mwili wa Hayati Magufuli ndiyo utapitishwa kuagwa.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar (japo ni nchi), Mwanza na Geita. Mara 5 ndiyo zilipangwa na Serikali kwamba, jeneza lenye mwili wa hayati Magufuli lizungushwe kwenye Uwanja wa Uhuru (Dar) na Uwanja wa Jamhuri (Dodoma) bila kusahau pale CCM Kirumba Mwanza.
Tarehe 25, ndiyo serikali ilisema itakuwa siku ya maziko ya mwili wa hayati Dk John Pombe Magufuli. Usisahau, Hayati Magufuli aliongoza nchi kwa Miaka mitano na miezi mitano.
MAKALA: OSCAR NDAUKA