
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaagiza watendaji wa serikali kujituma kufanya kazi akisisitiza kuwa atazinguana na watakaozingua.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 6,2021 wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakuu wa taasisi na Idara mbalimbali Ikulu Jijini Dar es Salaam.
“”Kwa hili nitatumia ule msemo wa Aweso, wewe ni kijana, mimi ni Mama, ukinizingua, TUNAZINGUANA…” kauli ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa mkurugenzi mkuu mpya wa Wakala wa Meli Tanzania (Tasac), Kaimu Abdi Mkeyenge na Watendaji wengine wote kwa ujumla walioapa leo.
Katika maelezo yake rais Samia amesema amemteua Mkeyenge kushika nafasi hiyo ili asafishe madudu yaliyopo kwenye taasisi hiyo.
“Ulikuwa ndani ya Tasac unayajua madudu yaliyopo. Jambo lililoniudhi zaidi kwa mwaka mmoja mmefanya vikao 23 vya bodi na imetumiwa karibu Sh 600 milioni, ukiangalia kilichozungumzwa na tija ya vikao hivyo hakuna.”
“Nataka ukafanye kazi na sio kwenda kupandisha mabega kwa wenzio uliowaacha, kama kuna makundi ukayaondoe, tunataka Tasac izalishe. Nasisitiza kafanye kazi ukinizingua tutazinguana,” amesema.
Rais Samia pia amempa miezi sita mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Erick Hamis kuhakikisha mambo yanakwenda kama inavyostahili.
“Sitegemei kama kuna mmoja wetu ataenda kinyume, nendeni mkafanya maamuzi. Mnachelea sana kufanya maamuzi. Mkitaka kufanya mkakwama njooni huku tuzungumze. Lengo ni kuikuza Tanzania yetu.