×

Waziri Ndumbaro Atembelea Kitalu cha Uwindaji cha Lake Natron East


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro ametembelea Kitalu cha Uwindaji wa Kitalii cha Lake Natron East kilichopo Wilayani Longido mkoani Arusha kilichokuwa kikimilikiwa na Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii ya Green Miles Safari Ltd kwa lengo la kukagua Kambi ya mwekezaji huyo, kusikiliza kero na maoni ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka kitalu hicho.

 

 

Ziara hiyo ya kikazi inafuatia Kampuni ya Green Mile iliyokuwa ikimiliki kitalu hicho na baadaye kufutiwa leseni mwaka 2019 kuwasilisha ombi la kufanyika kwa mapitio ya uamuzi uliotolewa.

 

 

Akiwa katika eneo la kitalu hicho ,Dkt. Ndumbaro amesema lengo la amejionea hali halisi katika eneo hilo na kuwaahidi wananchi kuwa maamuzi kuhusu suala hilo yatafanyika hivi karibuni baada ya kukamilika kwa taratibu za kusikiliza pande zote zenye maslahi na kitalu hicho.

 

 

“Nawaahidi wananchi, Serikali imewasikiliza wadau wote wanaohusika na suala hili wakiwemo viongozi wenu katika ngazi zote na wale wa wilaya, tambueni kuwa Serikali inawapenda na inawajali wananchi wake na ndio maana leo nimekuja hapa na Katibu Mkuu Dkt. Allan Kijazi na viongozi wengine,” amesisitiza Dkt. Ndumbaro.

 

 

Amewaeleza wananchi hao kuwa katika kufanya maamuzi kuhusu mgogoro uliopo Serikali lazima ifuate Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo kwa kuwa Tanzania inaongozwa kwa Misingi ya kufuata Sheria, hivyo amewataka wananchi hao wawe watulivu kabla ya kufanyika kwa maamuzi.

 

Aidha, Waziri Ndumbaro ameahidi kutoa uamuzi kuhusu mgogoro huo Aprili 15, 2021 Jijini Dodoma ambapo pande zote zinazohusika zitashiriki ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha uhusiano kati ya wawekezaji na wananchi ili kukuza sekta ya utalii hapa nchini.

 

 

Katika kikao cha kwanza kilichofanyika Jijini Dodoma , Waziri Ndumbaro alisikiliza pande zote katika mgogoro huo wakiwemo wamiliki wa Kampuni ya Green Mile, Viongozi wa Vijiji , Mweyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo ili kupata ukweli kuhusu mgogoro huo uliojitokeza baada ya kufutwa kwa leseni ya kitalu hicho.

 

 

Kwa upande wao wananchi wanaoishi Vijiji vinavyozunguka eneo la kitalu cha uwindaji cha Lake Natron wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema wanaimani na Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na wataendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo katika wilaya hiyo kupitia sekta ya wanyamapori.

 

Leave a Comment