
TANZANIA imeporomoka kwa nafasi mbili katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) vya mwezi Machi, mwaka huu vilivyotangazwa juzi Jumatano.
Licha ya Tanzania kuongeza pointi 1.05 kutoka zile 1087 ilizokuwa nazo hapo awali, imejikuta ikiporomoka kutoka nafasi ya 135 hadi ile ya 137.
Kipigo cha ugenini cha bao 1-0 ambacho timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilikipata kutoka kwa Equatorial Guinea katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) kimechangia kuwashusha.
Wakati Tanzania ikianguka kwa nafasi mbili, majirani zake Burundi wao wameporomoka kwa nafasi nne huku Rwanda wakipanda kwa nafasi nne.

Kufuzu Afcon kwa Ethiopia kunaonekana kumeibeba kwani imepanda kwa nafasi sita kutoka ile ya 146 hadi ya nafasi ya 140.
Kwa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Uganda iliyo nafasi ya 84, ndiyo kinara licha ya kushuka kwa nafasi moja ikifuatiwa na Kenya (102), Sudan (123), Rwanda (129) wakati zilizo mkiani ni Eritrea (203), Somalia (197) na Djibout (183).
Senegal iliyo nafasi ya 22 kidunia, inaendelea kuwa kinara kwa upande wa Afrika licha ya kuporomoka kwa nafasi mbili, ikifuatiwa na Tunisia, Nigeria, Algeria na Morocco.
STORI NA WILBERT MOLANDI,Dar es Salaam