
Staa wa Bongo Movies, Rose Ndauka ambaye kwa sasa pia anafanya muziki wa Bongo Fleva, leo Aprili 15, 2021 ametinga kwenye Studio za +255 Global Radio zilizopo Sinza-Mori jijini Dar na kutambulisha wimbo wake mpya wa Sijali aliomshirikisha Franshow.
Akifanya mahojiano kupitia Kipindi cha Bongo 255 amesema kuwa, ndoto za kuimba alikuwa nazo kabla ya kuanza uigizaji hivyo anafurahi kuzikamilisha kwa sasa huku akisema kuwa wasanii wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwenye jamii.
Akizungumzia drama zinazoendelea kwenye mitandao ya kijamii zikiwahusu wasanii wawili wa Bongo Fleva, Rayvanny na Harmonize, Rose amesema jamii itazichukua hizo kiki vibaya na zinawakosea wasanii heshima hivyo ni jambo la kuamua kama wanataka muziki ufanye vizuri au kuendelea na kiki.
“Hapo ni sisi tunapaswa kuchagua kama tunataka skendo au tunataka muziki wetu ufike mbali. Lakini kiukweli hayo mambo yanawaathiri wale ambao wanautegemea muziki kama sehemu ya kipato hivyo hayo mambo yanawaharibia wengine,” anasema Rose.

Rose ambaye ni mama wa watoto wawili, amesema anaamini kwa kuingia kwenye muziki ambapo ameshatoa wimbo mmoja wa Sijali wenye mahadhi ya Hip Hop atakuwa amewaonesha upande wa pili mashabiki wake wanaomfuatilia katika uigizaji na kuahidi kuwa hatawaangusha huku akiwaomba wampe sapoti kwa kuwa bila wao hawezi kusonga mbele .
“Nawaomba mashabiki wangu walionikubali katika filamu hadi leo kuwa na umaarufu niliokuwa nao, wanisapoti pia kwenye muziki wangu ili niendelee kuja na mambo mazuri na kuwa mmoja watu wenye mchango katika muziki wa Tanzania,” amesema msanii huyo.
Wakati kuhusu matarajio yake katika muziki huo amesema kuwa, ni kuja kufanya kazi na wasanii wengine akiwemo Rosa Ree, Shilole na wengine waliomo kwenye muziki huo.
Kuhusu maneno ya kuwepo kwa ugumu katika muziki huo na hususani kwa wasanii wa kike, Rose amesema yeye haoni ugumu isipokuwa anaamini ni juhudi za msanii na sapoti kutoka kwa watu na ndiyo maana wengine wapo hadi leo.
“Hakuna cha ugumu katika kazi yeyote, ni wewe tu kujiwekea mikakati ya namna gani ya kufanya kazi yako kwa ubora na watu kukukubali na kukusapoti, ndiyo maana pia nimeomba sapoti kutoka kwa watu ili niwezi kutimiza azma yangu hii ya kuielimisha jamii kupitia muziki,”anasema Rose
⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx