
Mbunge wa zamani Jimbo la kigoma kusini, David Kafulila amewata baadhi ya wanasiasa wanaotaka kupenyeza ajenda zao binafsi kwa Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu kuacha kufanya hivyo kwani kuna mambo ya msingi ya kujenga taifa.
“Uamuzi wa Bunge kushauri ATCL iendelee au isiendelee kununua ndege unapaswa kufikiwa baada ya ushauri wa kitaalamu kuhusu biashara hii. Lazma wajue asilimia ngapi ya hasara inatokana na udhaifu wa taasisi na ngapi inatokana na sababu nje ya kampuni.
“Lazma kujua kwa nini nchi kama Kenya, Rwanda au Afrika Kusini wanaendelea na bila hasara ya kihasibu? Ingawa tunapata hasara ya kihasibu (accounting loss) ATCL, je, tunapata faida za kiuchumi kiasi gani (Economic Profit)?
“Je, mpango wa ATCL ilikuwa kuanza kupata faida baada ya miaka mingapi? Yote haya yanahitaji wataalamu wa Airline Industry kusaidia ufahamu kabla ya maamuzi ya kuendelea kununua ndege ama kusitisha..
“Upinzani unaonesha matumaini makubwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan nadhani ndio siri ya mafanikio ya CCM ilipo. Siri ya CCM kudumu madarakani ni uwezo wake wa kujibadilisha kukidhi mahitaji ya wakati. Hali ilikuwa hivyo alipoingia JK na hata alipoingia JPM.
“Labda Prof. Muhongo alimaanisha Serikali isiendelee kuwekeza kwenye miradi ya maji maana sidhani kama msomi anaweza kupendekeza tuachane na mradi wa Bwawa la Nyerere kwa hatua uliofikia.
“Kama ushauri ni tusiendelee kuwekeza kwenye miradi ya umeme wa maji sioni tatizo kwa maana nchi inapokuwa na vyanzo tofauti kama upepo, jua, gesi na joto ardhi ni ushauri sahihi kitaalamu kwa maana utegemezi kwa chanzo kimoja ukiwa mkubwa sio salama sana!
“Hoja ya kwamba tuachane na mradi uliokwishafikia hatua kubwa wa Bwawa la Nyerere hauwezi kuwa sahihi na dunia itatushangaa.
“Rais Samia ni wa aina yake, amekuja wakati ambao tafiti nyingi zinathibitisha uwezo mkubwa wa wanawake kiuongozi duniani.
“Rais Samia ni wa aina yake, Ripoti ya WOMEN COUNT 2020 inaonesha katika makampuni makubwa 350 soko la mitaji London, kampuni ambazo walau 30% ya wajumbe wa Bodi ni wanawake zilipata faida mara 10 zaidi ya kampuni ambazo wajumbe wa Bodi wanawake ni wachache mno.
“Kuhusu ripoti ya CAG, baada ya Kamati za Hesabu za Serikali (PAC, LAAC) kuwahoji maofisa masuuli, baadhi ya hoja zitafutwa maofisa hao wakipotoa maelezo na vielelezo vya kuridhisha. Maelezo yasipojitosheleza Kamati hupeleka taarifa bungeni kwa ajili ya maamuzi ya Bunge.
“Ni bahati mbaya kwamba baada ya hoja (Ripoti ya CAG) kufutwa huwa hakuna mjadala sana kwenye Umma. Lakini zipo ambazo huwa zinafutwa kutegemea maelezo na vielelezo vya maofisa masuuli mbele ya Kamati za Hesabu za Bunge.
“CAG wote walifanya kazi kwa weledi, tangu ndugu Utouh, Prof. Assad na sasa ndugu Kichere. Mara zote ripoti hizo ziliondoka na watu. “Pamoja na kupiga hatua katika kupunguza rushwa na ufisadi, kwa mujibu wa Ripoti za Transparency International, bado tatizo ni kubwa na hivyo ni vita ya kudumu.
“Ufisadi haujawahi kwisha na sio rahisi kuumaliza kabisa bali kuupunguza, ndio sababu ni moja ya agenda katika agenda 10 za Rais wa awamu ya sita, Mama Samia. “Hoja kwamba kuna CAG alipata kunyimwa nyaraka baadhi katika kutimiza majukumu yake ya ukaguzi zinasikitisha na pengine ni jukumu la Bunge kufanyia kazi,” amesema Kafulila.