
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesitisha shughuli za usafiri wa baharini zikiwemo safari za meli na vyombo vingine vya usafiri baharini kuanzia leo jumamosi Aprili 24, saa tatu asubuhi hadi pale taarifa nyingine zitakapotolewa na mamlaka husika.
Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa pili wa rais Dkt. Khalid Salum Mohamed amesema serikali imefikia uamuzi huo ili kuchukua tahadhari ya kimbunga Jobo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, amesema kuwa hadi kufikia tarehe 25/04/2021 kimbunga hicho kitakuwa kimetua maeneo ya Dar es Salaam na mara kinapotua hupunguza nguvu sana.
Aidha Mamlaka ya hali ya hewa nchini TMA imewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuzingatia mwelekeo wa upepo na mawimbi ya bahari katika maeneo husika.