×

Harmo Amuibulia Kimbunga Mondi

AMEMUIBULIA kimbunga, lakini siyo kile cha Jobo! Ndivyo wasemavyo mashabiki wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide baada ya bosi wao, Rajab Abdul ‘Harmonize’ kuweka rekodi za kila aina ndani na nje ya Bongo, IJUMAA WIKIENDA lina ripoti maalum.Kupitia wimbo wake mpya wa Attitude aliowashirikisha mwanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Awilo Longomba na msanii wa kitambo wa Bongo Fleva, Hamis Baba ‘H-Baba’, Harmonize amethibitisha ubora wake.

 

ATIKISA REKODI YA MONDI

Ni rasmi sasa kwamba Harmonize au Harmo ametikisa rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na bosi wake wa zamani kunako Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na kuwasababishia presha kubwa mashabiki wake.

Diamond au Mondi alikuwa na rekodi ya kipekee aliyoiweka kupitia wimbo wake wa Waah aliomshirikisha maestro wa muziki wa Rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mopao Koffi Olomide, mwishoni mwa mwaka jana.

Kwenye Mtandao wa YouTube, Harmo kupitia wimbo huo wa Attitude amefanikiwa kuweka rekodi ya kufikisha zaidi ya watazamaji laki 1 ndani ya dakika 44 pekee na kuvunja rekodi ya Mondi ambaye yeye wimbo wake wa Waah ulifikisha zaidi ya watazamaji laki moja kwa muda wa saa moja.

 

ARUSHA KIJEMBE

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmo aliwakumbusha mashabiki wake kwamba, kwa sasa ndiye anayeshikilia rekodi hiyo na si msanii mwingine yeyote.Alirusha kijembe; “Ni rekodi mpya kwenye kiwanda cha muziki, dakika 44, watazamaji laki 1, maana binadamu kwa kusahau…!!! Hatujambo…!!!

 

MONDI KUJIBU MAPIGO

Kufuatia kijembe hicho ndipo mashabiki wa Mondi wakamgeukia na kushambuliwa kwa maneno akitakiwa kujibu mapigo kwa kuachia wimbo mkali utakaofuta rekodi hiyo ya Harmo.Harmo ameendelea kuwashukuru wale wote waliofanikisha mchongo huo wa kolabo na Awilo na H-Baba.

 

“Shukurani za kipekee ziende kwa kaka yangu Master Garzy kwa rekodi hii, siwezi kumaliza kumshukuru kwa kubariki sauti hii, amekuwa rafiki mzuri na kaka, watu wengi wanajiuliza kwa nini H-baba? Nilikuwa shabiki wa H-Baba kabla hajawa shabiki yangu na kuwa kaka kwangu, nikisikia sauti yake namsikia kama DJ Arafat (marehemu) aliyebakia Afrika…!!!!

“Nadhani leo dunia inajionea, nikimzungumzia Awilo Longomba ndiye mkongwe mwenye nyimbo kubwa nyingi Afrika..!!!“Nimeanza kujua muziki miaka ya 1998, nyimbo za Awilo ndizo za moto…!!!! Nilipomwambia mama nimefanya ngoma na Awilo hakuniamini mpaka alipousikiliza kwa hiyo kuwa makini unaweza ukawa unachukia kumbe huko nyumbani bimkubwa wako ni sikukuu…!!!” Alisema Harmo.Anasema amekua akiwa anasikiliza nyimbo wa Awilo na ilikuwa ni moja ya ndoto zake kwamba siku moja afanye wimbo na jamaa huyo, jambo ambalo sasa limefanikiwa.

 

MAMA YAKE ASHINDWA KUAMINI

Anaendelea kusema kuwa, hata mama yake hakuamini alipomuambia amefanikiwa kufanya kolabo na Awilo.

 

SINTOFAHAMUHata hivyo, wimbo huo ulipofikisha watazamaji laki 9, walishuka ghafla hadi laki 7, jambo lililoibua sintofahamu ya huwenda kuna mtu alitaka kumfanyia mchezo mchafu.

 

UFAFANUZI

Hata hivyo, mmoja wa watu wenye utaalam juu ya ishu hiyo alitoa ufafanuzi;“Hakuna mtu anaweza kushusha views (idadi ya watazamaji) za mtu YouTube. “Ni hivi; views hazijafika tu. Asiyekubali kushindwa si mshindani. Hao Wasafi washushe views wao ndiyo wenye YouTube? Ama? “Halafu vitu vingine tusipende kudanganyana. Tatizo tunataka kumshindanisha Harmo na Dai (Mondi).

 

Hiyo kitu haipo. Harmo tumshindanishe na Rayvanny ila Harmo anamshinda Rayvanny.“Ila kwa Diamond hapo tunakuwa wote wajinga. Diamond hana mpinzani Afrika Mashariki na Kati. Inauma ila ndiyo ukweli.“Huo wimbo mpya ni mzuri sana ila haupo consistent (hauna uwiano). Diamond anachowashinda wanamuziki wetu wengi ni kuwa nyimbo zake zinakuwa nzuri kuanzia mwanzo hadi mwisho.

 

“Hiyo new song ya Harmo ina sehemu nzuri balaa, halafu sehemu zingine zimepoa mno. Wajifunze kuwa na wimbo unaonoga mwanzo hadi mwisho, siyo tu kisehemu kidogo kizuri.“Kwa kuwaelezea tu, kinachofanya views kushuka ni kwamba kuna watu wanadanganya; yaani mtu huyohuyo anaangalia wimbo sehemu tatu hivyo views zinapanda, baadaye YouTube wanapitia IP address wanaona waliojaribu kudanganya ndiyo wanawaondoa. Na wakati mwingine mtu ananunua views so baadaye YouTube wakipitia wanaondoa zilizonunuliwa.”

 

ATTITUDE YA HARMO

Hadi jana, video hiyo ya Wimbo wa Attitude ilikuwa na watazamaji zaidi ya milioni 3.5 ndani ya siku moja, rekodi ambayo ni ya kipekee kuwekwa na msanii wa Bongo Fleva.

 

WAAH YA MONDI

Kwa upande wake, video ya Wimbo wa Waah wa Mondi ilitoka Novemba 30, 2020 ambapo yenyewe ilijikusanyia watazamaji laki 1 kwa muda wa saa moja.Pia Waah iliweka rekodi ya kufikisha watazamaji milioni moja kwa saa 8 na milioni 2 kwa saa 13 pale mjini Youtube. Ndani ya miezi minne, video hiyo ya Waah ina watazamaji zaidi ya milioni 60.

 

PEPETA YA RAYVANNY

Rekodi nyingine ambayo pia imevunjwa na Harmo ni ile iliyokuwa inashikiliwa na memba mwingine wa Wasafi, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ kupitia wimbo wake wa Pepeta.Video ya Pepeta iliachiwa Septemba 2019 na kuweka rekodi mpya kwenye muziki wa Afrika akiwa ameshirikiana na mwimbaji na mwigizaji wa Bollywood, India aitwaye Nora Fatehi ambapo ilipata watazamaji milioni moja ndani ya saa 6.

Leave a Comment