×

Serikali Yaandaa Muswada wa Uvunaji, Upandikizaji Figo za Binadamu

SERIKALI imesema kuwa hadi Aprili 2021 hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zimeshapandikiza figo kwa watu 80.

 

Takwimu hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel , Bunge limeelezwa leo Jumatano Aprili 28, 2021, wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Rose Tweve bungeni mjini Dodoma.

 

Naibu waziri huyo amesema Muhimbili wamepandikiza figo 62 na Benjamin Mkapa figo 18.

 

Katika swali la nyongeza Tweve alihoji ni lini Serikali itakuja na muswada wa kuruhusu biashara ya kuvuna viungo ili kuwanusuru Watanzania wanaopoteza maisha kwa kukosa viungo.

 

“Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha utaratibu maalum wa kuvuna viungo kama figo na moyo kwa ajili ya Watanzania wenye uhitaji wa viungo hivyo,” amehoji Tweve.

 

Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel, amesema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya upandikizaji wa viungo Nchini, Serikali imeandaa Muswada wa kutunga Sheria itakayoongoza taratibu za uvunaji, utunzaji na upandikizaji wa viungo.

 

Naibu Waziri ameeleza, “Kwa kuwa huduma zimeanza kutolewa, kwa sasa nchi inatumia miongozo ya kimataifa kusimamia uvunaji na upandikizaji wa viungo…”

 

Leave a Comment