
Mwanaanga za juu wa Marekani, Michael Collins, ambaye aliongoza Apollo 11 wakati wanaanga wenzake wawili walipokuwa binadamu wa kwanza kutembea mwezini, amefariki jana Jumatano kwa saratani, familia yake imesema.
Collins, ambaye wakati mwingine hujulikana kama “binadamu mpweke katika historia” kutokana na kuwa pekee kwa muda mrefu chomboni katika anga za juu wakati wenzake wakitembea katika uso wa mwezi, hakupata umaarufu duniani kama wa Neil Armstrong na Buzz Aldrin waliotua.
Lakini alisifika kama mtetezi wa mpango wa kufanya uchunguzi wa anga za juu: akionyesha ujuzi na ujanja na bado hakutaka sifa, huku akisisitiza katika mahojiano na NASA kuwa kwa asilimia 90 mafanikio yake hayakuwa na uhakika na yalikuwa ya bahati na kwamba wanaanga za juu hawatakiwi waonekane kuwa mashujaa.
“Mara zote Mike alikabiliana na changamoto kwa upole na unyenyekevu, na amelikabili hili, changamoto yake ya mwisho,” familia ya Collins ilisema katika ujumbe wake uliotumwa Twitter.

Mwanaanga mwenzake, Aldrin aliongoza maombolezo, akiandika katika akaunti ya Twitter akisema: “Mpendwa Mike, kokote ulikokuwa au utakakokuwa, wakati wote utakuwa na moto wa kutupeleka katika viwango vipya. Tutakukumbuka. Pumzika kwa amani.”
Rais wa Marekani, Joe Biden alisema wakati Collins “anaweza kuwa hakupata kuenziwa sawa na wengine,” alikuwa “mshirika sawa, akilimbusha taifa letu kuhusu umuhimu wa ushirikiano katika huduma ya malengo makubwa.”
Collins alisema mwaka 1930 jijini Rome na baba yake alikuwa ofisa wa jeshi wa Marekani aliyekuwa nchini Italia akifanya kazi ubalozini. Baadaye Collins akawa rubani wa ndege za kivita na rubani wa majaribio wa kikosi cha anga.
Aliomba kujiunga na NASA baada ya kuvutiwa na John Glenn, Mmarekani wa kwanza kwenda katika mzingo wa dunia, na alichaguliwa kuwa mwanaanga za juu mwaka 1963.
Safari ya kwanza katika anga za juu ilikuwa katika mpango wa Gemini 10, ambako aliweka rekodi ya wakati huo ya kutembea katika anga za juu.
Lakini anajulikana zaidi kwa kuwa mmoja wa wanaanga za juu wa chombo cha Apollo 11 wakati Julai 20,1969 wanaanga wake wawili, Neil Armstrong na Buzz Aldrin walipiga hatua kubwa katika historia ya binadamu.